Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Rais Samia ashiriki kongamano la nishati Norway

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi zilizoendelea kushirikiana na nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ili kuwezesha uzalishaji wa nishati salama kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani

Mhe. Rais Dkt. Samia ametoa kauli hiyo wakati akihutubia Kongamano la Nishati la Oslo lililofanyika jijini Oslo, Norway leo tarehe 14 Februari 2024.

Mhe. Rais Samia amesema nchi zinazoendelea zina malighafi nyingi za kuzalisha nishati safi huku nchi zilizoendelea zina teknolojia ambayo inaweza kutengeneza malighafi hizo kuwa nishati safi kwa matumizi ya binadamu na kulinda mazingira.

Aidha, amesema Tanzania inaendelea kuzikumbusha nchi zilizoendelea kutimiza ahadi ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu ili kufikia lengo la kupunguza gesi hiyo kwa asilimia 43 ifikapo mwaka 2030 na kufikia lengo la kupunguza ongezeko la joto duniani kufikia nyuzi joto 1.5.

Amesema kwa upande wa Tanzania nishati safi inapatikana kutokana na jua, upepo na maji na pia madini mbalimbali ambayo yanaweza kuzalisha nishati safi na kutumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kwenye eneo la teknolojia ya kubadilisha malighafi hizo kuwa nishati safi.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Norway, Mhe. Jonas Gahr Store amesema nchi yake ambayo imepiga hatua kubwa kwenye matumizi ya nishati safi na mbadala itaendelea kushirikiana na nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ili kuziwezesha nchi hizo kuondokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za kiafya hususan kwa wanawake zinazotokana na matumizi ya nishati chafu ikiwemo mkaa na kuni.

Kongamano la Nishati la Oslo limewashirikisha wadau mbalimbali wa mazingira akiwemo Mjumbe Maalum wa Rais wa Marekani kwenye masuala ya Mazingira, Mhe. John Kerry

Norway ni nchi ya kwanza katika kusafirisha gesi asilia katika nchi za Ulaya na ya nne duniani katika kusafirisha gesi hiyo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *