Wazazi mkoani Mwanza wameaswa kuzingatia malezi ya watoto wao

Wazazi wametakiwa kuwa makini hasa katika suala la malezi ya watoto wao hii ikiwa ni kutokana na uwepo wa teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa inaonekana kuchangia kuharibika kwamaadili ya watoto.

Hayo yameelezwa na Katibu Tawala Msaidizi wa Utawala na Rasilimali watu Bw.Daniel Machunda wakati akizungumza kwenye kikao kazi cha kutathmini malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ambapo amesema msingi imara wa malezi ya mtoto unaanzia katika ngazi ya familia na endapo eneo hilo litakuwa na mapungufu basi linaweza kuchangia kuharibika kwa mtoto.

“Ndugu zangu washiriki wa kikao kazi hiki nawaombeni sana mkalifanyie kazi jambo hili, Dunia sasa imekumbwa na changamoto nyingi hasa mabadiliko ya teknolojia,vitendo vya ukatili pia na umasikini,mkazo wa elimu kwa familia ni lazima uzingatiwe”,Machunda

Katika hatua nyingine Machunda amesema bado familia nyingi haziwajibiki ipasavyo katika malezi ya watoto wao kotokana na wawazi wengi kuwekeza muda mrefu katika shughuli za kimaendeleo bila kutenga muda wa kulea familia.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum anayeshughulikia dawati la watoto Merry Shilla amesema katika jamii ya sasa bado kumekuwa na vitendo vya ukatili ambavyo vinafanywa dhidi ya watoto na hii inatokana na kukosa malezi mazuri ya wazazi hivyo kwa kutambua umuhimu wa malezi ya watoto wamejipanga kuwajengea uwezo Maafisa wote wanaoshughulikia watoto katika ngazi zote za Mikoa ili kuondoa vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikifanywa kwa watoto.

“Bado kumekuwa na vitendo vya ukatili kwa watoto na pia kukosa malezi imara kutoka kwa familia, hizi changamoto hatuna budi kukusanya nguvu kwa pamoja ili kukabiliana nazo”,Shilla

Kikao kazi hicho cha tathimini kimewashirikisha Maafisa Ustawi wa Jamii,Maendeleo ya Jamii,Maafisa Lishe,Mipango na Waganga wakuu wa Wilaya kutoka Halmashauri ya Ilemela, Nyamagana, Magu, Kwimba, Misungwi, Sengerema, Ukerewe na Buchosa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *