Wanawake wanaojishugulisha na uchimbaji mdogo wa madini Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wamesema kuwa wanakumbuna na changamoto nyingi katika shughuli za uchimbaji ikiwemo kuwa na mitaji midogo hali inayowafanya waombwe rushwa ya ngono ili kukidhi mahitaji katika sekta ya uchimbaji wa madini.
Hayo wameyasema leo wakati wakizungumza na Jambo Fm ilipotembelea katika maeneo tofauti ya machimbo madogo ya dhahabu Wilayani Kahama kufuatilia changamoto wanazokutana nazo wanawake wanaofanya shughuli za uchimbaji mdogo katika wilaya hiyo.
Wanawake hao wamesema kuwa kutokuwa na mitaji ya kutosha kunafanya waingie katika vishawishi vya rushwa ya ngono ili kuweza kupata mitaji huku wakiiomba serikali kuruhusu mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa elimu migodini pamoja na kuandaa sera na sheria zitakazowasaidia wanawake katika sekta ya uchimbaji wa madini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mgodi wa Ntambalale namba 4 uliopo halmashauri ya Msalala Zacharia Soko amesema kuwa ili wanawawake wanaojishughulisha na uchimbaji mdogo waondokane na rushwa ya ngono serikali iwape kipaumbele kwenye mikopo ili wapate mitaji na kuwatengenezea vikundi na kutoa wito kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji kote nchini kuwapa nafasi wanawake katika sekta ya uchimbaji bila kuangalia jinsia zao.
Awali akiongea na Jambo FM Afisa Mawasiliano wa Shirika lisilo la kiserikali linaloshughuLika na Mafuta, Madini na Gesi, Shakira Zaidi amesema kuwa shirika lao limeamua kuja na mradi unaolenga kuibua changamoto ambazo wanapitia wanawake katika uchimbaji mdogo wa madini ili kuwasaidia wanawake na kutatua changamoto zao ikiwa ni pamoja na kuwatengenezea sera na sheria za kuwaongoza katika sehemu zao za uchimbaji.