Aliyemuua mpenzi wake  Marekani akamatwa  Kenya

Polisi nchini Kenya wamesema wamemkamata tena mwanaume ambaye hatua yake ya kutoroka gerezani ilizua mjadala kwenye taifa hilo baada ya awali kukamatwa kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake nchini Marekani.

Kevin Kang’ethe alizuiliwa akisubiri kurejeshwa nchini Marekani kutokana na kifo cha Margaret Mbitu, ambaye mwili wake ulipatikana katika maegesho ya magari ya uwanja wa ndege mwaka jana, lakini akatoroka kutoka kituo cha polisi wiki iliyopita kwa njia isiyoeleweka.

Kamanda wa polisi Jijini Nairobi  Adamson Bungei, amesema Kang’ethe alikuwa amejificha katika nyumba ya jamaa yake viungani mwa jiji la nairobi, ambapo polisi walimpata jumanne jioni baada ya msako wa siku kadhaa.

Kwa mujibu wa maofisa wa usalama, kwa sasa mshukiwa  amefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kutoroka kizuizini wakati akisubiriwa kurejeshwa nchini Marekani.

Hati ya kukamatwa kwa Kang’ethe ilitolewa baada ya kutoroka Marekani kuelekea nchini kwao Kenya, ambako alikamatwa mwishoni mwa Januari, ambapo maafisa wanne wa polisi, jamaa wawili na wakili wa mshukiwa walikamatwa kuhusiana na kutoroka kwake gerezani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *