Wananchi watakiwa kujiandikisha katika daftari la Wapiga Kura

Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Shaban Itutu, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji na uboreshaji wa daftari la wapiga kura ili kupata viongozi bora.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Kiseke A jijini Mwanza, Itutu amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kila mwananchi mwenye sifa za kushiriki uchaguzi huo ili aweze kuchagua kiongozi ambae anaona ana uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

“wito wangu ni wananchi kujitokeza kwenda kuboresha taarifa zao katika daftari la mpiga kura kwa sababu wasipoenda watakosa haki ya kushiriki katika uchaguzi huo na ukiangalia ili kumpata kiongozi bora ni lazima uwe umejiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura”

Itutu amesema Chama cha ADC kimejipanga kuleta mabadiliko makubwa katika jamii na jambo hilo linawezekana endapo wananchi watajitokeza kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura na kuwachagua viogozi wa chama hicho.

Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo pia ameiomba serikali kupunguza bei ya nishati ya gesi ya kupikia ili kila mwananchi aweze kumudu gharama zake jambo ambalo litasaidia kupunguza ukataji wa miti hapa nchini.

“nchi yetu imekua ikikatwa sana miti lakini tumekua tukisisitiza kutokutumia mkaa lakini kwa bahati mbaya bado gesi ina gharama kubwa hivyo jambo kubwa ni kupunguza bei ya gesi kwa sababu tunaipata hapa nchini ili wanananchi waweze kununua mtungi wa gesi hata kwa shilingi elfu tano badala ya elfu ishirini na tano”

Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mwanza akiwemo Alfred Kabuga pamoja Gloria Jekonia wameonyesha nia ya kushiriki katika uchaguzi huo ambapo wamesema wako tayari kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi, huku wakisisitiza wananchi wa maeneo mengine kuchagua viongozi bora kwa maendeleo yao na maslahi mapana ya taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *