El-nino na maporomoko ya Hanang’ chanzo cha Kusuasua kwa utekelezaji wa miradi nchini – Dk. Mwigulu

Serikali kupitia Wizara ya fedha imesema kusuasua kwa baadhi ya miradi nchini kumetokana na kushuka kwa upelekaji wa fedha katika miradi hiyo hatua iliyosababishwa na majanga mbalimbali yaliyotokea hivi karibuni ambayo yaliharibu utaratibu mzima wa bajeti ya mwaka 2023/24.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha Dk.Mwigulu Nchemba wakati akiwa katika ziara yake jijini Mwanza.

Dk. Nchemba amesema majanga mbalimbali yaliyotokea nchini ikiwemo mafuriko yaliyosababishwa na mvua ya el-nino, maporomoko ya Hanang’ ,Mbeya, Lindi na Mtwala iliharibu mtiririko wa fedha zilizopangwa katika bajeti ya 2023/24.

“Kumekuwa na mtiririko hafifu wa utolewaji wa fedha katika baadhi ya miradi hii ni kutokana na majanga hayo yaliyoathiri bajeti yote ya mwaka jana na kusababisha serikali ianze kuhudumia maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kurejesha miundombinu na makazi ya watu ambako haikuwa imepangiwa,” Dk. Nchemba.

Aidha amesema tayari Wizara hiyo imewasiliana na wizara ya maji ambayo muda si muda mrefu itaanza kusambaza fedha hizo ili miradi iliyokwama ikamilishwe kwa wakati.

Waziri Dk.Nchemba alitembelea na kukagua ujenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kanda ya Ziwa chuo ambacho ujenzi wake ulianza Januari, 22, 2022 ukigharimu zaidi ya Sh.bilioni 7.8.

Akizungumzia ujenzi wa Kampasi hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Nchini (TIA), Profesa William Pallangyo amesema umefikia asilimia 99 na kukamilika kwake kutasaidia kuwahudumia kwa wingi wananchi wa mikoa ya kanda ya ziwa na kuachana na utaratibu uliopo wa kupangisha.

“Kampasi hii inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Oktoba 12, 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan huku ikiwa na uwezo wa kuwahudumia zaidi ya wanafunzi 2430 kwa wakati mmoja tofauti na hapo awali walipokuwa wakitumia majengo ya kupanga.

Aidha Waziri wa Fedha Dk. Nchemba ameonesha kuridhishwa na utekelezwaji wa mradi huo kwa kuwa umekidhi vigezo ikiwemo miundombinu yake iliyozingatia sifa na mahitaji ya kila mwanafunzi hata wale wenye ulemavu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *