Wakazi wa mtaa wa Mwatulole eneo maarufu la Savana kata ya Buharahara Halmashauri ya Mji wa Geita Mkoani Geita wamejikuta wakimwaga machozi wakishinikiza serikali kuwarekebishia barabara yenye urefu wa mita 200 iliyopo katika eneo lao wakidai haijarekebishwa kwa kipindi cha miaka 10 ambayo imekuwa chanzo cha kusababisha maji kujaa kwenye makazi yao wakati wa masika.
Wakizungumza na Jambo Fm wananchi hao wamesema eneo hilo limekuwa korofi hasa kipindi cha mvua kwani maji hujaa barabarani na kusambaa kwenye makazi ya watu ambapo kaya zaidi ya 100 huathirika kutokana na kutelekezwa kwa mda mrefu huku wakiiomba serikali kuingilia kati changamoto hiyo kwani kipindi cha masika huwa hatarini kupata magojwa ya mlipuko.
Wananchi hao wamesema hapo awali walichangishwa fedha kiasi cha shilingi elfu 10 kila kaya kwa ajiri ya kurekebisha barabara hiyo lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Geita Mhandisi Bahati Subeya amekiri uwepo kwa changamoto hiyo na kusema kuwa katika bajeti ya fedha ya mwaka 2024/25 TARURA haijatengewa fedha kwa ajiri ya ukarabati wa barabara hiyo hivyo barabara hiyo litarekebishwa kulingana na upatikanaji wa fedha.