Nyoka na Kenge waingia kwenye makazi ya watu, wananchi wahofia usalama wao.

Wananchi wanaoishi jirani na mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege mtaa wa Bondeni kata ya Kamunyonge manispaa ya Musoma mkoani Mara,wamelalamikia vichaka vilivyopo kandokando ya mradi huo wakidai ni maficho ya nyoka na kenge ambao huingia kwenye nyumba zao na kuhatarisha usalama.

Mbali na hilo,Bw.Julius Mwamba na Salome Mwita wamehoji ni lini watalipwa fidia zao zitokanazo na kupisha maeneo yao kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo wa ndege ambapo wamesema imekua ni muda mrefu tangu serikali ilipofanye uthamini hali inayofanya washindwe kuendeleza maeneo yao.

Meneja wa uwanja wa ndege mjini Musoma FRANK MSOFE amesema maeneo yote ya mradi yaliyo jirani na makazi ya wananchi yatasafishwa kikamilifu huku akiwatoa hofu wale wote walioachia maeneo kwa ajili ya kupisha mradi huo,watalipwa stahiki zao baada ya mchakato mzima wa uthamini kukamilika.

Hoja za wananchi zimeibuka wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika mtaa wa Bondeni kata Kamunyonge mjini Musoma uliowakutanisha pamoja wananchi na viongozi wa kada mbalimbali ili kusikiliza na kutatua kero za wakazi wa kata hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *