Na Melkizedeck Anthony
Madereva wa boda boda mkoani Mwanza wametakiwa kuvaa kofia ngumu na kufuata Sheria za usalama barabarani pindi wanapotumia pikipiki zao ili kuepukana na ajali ambazo zinaweza kutokea.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Mwanza Mrakibu wa Polisi (SP) Sunday Ibrahim wakati akitoa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha boda boda wa vituo mbalimbali vya wilaya ya Nyamagana ambapo amesema elimu hiyo imelenga kuwapa uelewa makundi mengine ya watumiaji wa barabara hususan bodaboda.
Sunday ameongeza kuwa jeshi hilo kupitia kikosi cha Usalama barabarani litamchukulia sharia kali mtu yeyote atakaye kwenda kinyume na sheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wale wote watakao kamatwa wakiwa hawajavaakofia ngumu.
“wengi mnasema abiria hataki kuvaa kofia ngumu lakini afisa msafirishaji mzuri na wa kisasa wa Mwanza atampa elimu kabla ya kuondoka juu ya umuhimu wa kofia ngumu” amesema SP Sanday.
Kwa upande wake mwenyekiti wa waendesha pikipiki wilaya ya Nyamagana Mohamed Iddy amewataka waendesha bodaboda hao kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani yeyote anae kosea kuna sheria itakayo muhukumu hivyo, ni wajibu wa kila mmoja kumlinda mwezake ili kazi hiyo iendelee kuwa nzuri.
“Kujichukulia sheria mikononi unaweza kupoteza haki yako hivyo tuziache mamlaka zifanye kazi zake” amesema Mohamed Idd.
Nae koplo wa Polisi wa kikosi Cha usalama barabarani mkoani humo Rehema Juma amewataka madereva wa bodaboda kuzingatia Sheria za usalama barabarani kwa kuacha kupakia abiria zaidi ya mmoja katika pikipiki zao .
“sheria ya usalama barabarani inatukumbusha mara zote hasa unapoingia barabarani kwani alietengeneza chombo hiki amekipa uwezo wa kubeba abiria mmoja kwenye hiyo pikipiki maana yake ni nini anajua pikipiki hiyo itakapopata shida utapata namna ya kumudu hicho chombo” amesema Koplo Rehema.