Mahakama ya wilaya ya Itilima mkoani Simiyu imemhukumu Jegi Msalenge (20) kwenda jela miaka 30 na kulipa fidia ya shilingi 300,000 kwa mhanga baada ya kupatikana na hatia ya kubaka mtoto mwenye umri wa miaka 16 ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili na kumsababishia maumivu pamoja na ujauzito.
Awali mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya taifa ya mashtaka wilaya ya Itilima, mkaguzi msaidizi wa polisi Vedastus Wajanga, aliieleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 15 na 28, 2023 katika kijiji cha Sagata, ambapo katika siku hizo mshtakiwa akiwa anachunga ng’ombe kwa ndugu yake kijini hapo alitenda kosa hilo la kubaka.
Mwendesha mashtaka huyo amesema kuwa taarifa hizo zilifika katika kituo cha polisi wilaya ya Itilima Septemba 4 mwaka huu na Septemba 18 mwaka huu mshtakiwa alifikishwa mahakamani na kusomewa kosa lake na jumla ya mashahidi wanne na kielelezo kimoja kilitolewa na upande wa mashtaka na mahakama hiyo ilimtia hatiani mshtakiwa huyo.
Upande wa mashtaka uliomba apewe adhabu kali ili iwe funzo kwake na jamii kwani matukio kama hayo huacha kumbukumbu mbaya isiyofutika kirahisi katika maisha ya mhanga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na mhanga ana ujauzito unaosababisha mtoto kuzaa mtoto mwenzake.
Hakimu mkazi mwandamizi wa wilaya ya Itilima Robert Kaanwa baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka amemhukumu kwenda jela miaka 30 na kulipa fidia ya shilingi 300,000.