Mwanasiasa Mkongwe Nchini, Dkt. Willbroad Slaa (76) ameiomba Mahakama ya Rufani ya Tanzania masijila ya Dar es Salaam kupitia hati ya dharura impatie dhamana wakati akisubiri kusikilizwa kwa rufaa yake ya jinai.
Ombi la Dkt. Slaa limewasilishwa hii leo Februari 21, 2025 chini ya hati ya dharura na Wakili wake aliyedai mteja wake amewekwa rumande kinyume cha sheria huku Afya yake ikiendelea kuzorota licha ya kuwa kosa linalomkabili linastahili dhamana.
Amesema, “kufungwa kwa Dkt. Slaa katika Gereza la Keko ni kitendo kinachosababisha madhara yasiyorekebishika. Kwa misingi hiyo, tunaiomba Mahakama itoe uamuzi wa haraka juu ya maombi haya ya dhamana.”

Hata hivyo, kinachosubiriwa ni Mahakama ya Rufani kupanga taratibu za usikilizwaji wa shauri hilo ambalo limezua hisia mseto, baada ya Dkt. Slaa kunyimwa dhamana kwa kosa lenye dhamana.
Dkt. Wilbroad Slaa alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akishitakiwa kwa kosa moja la kuchapisha taarifa ya uongo katika mtandao wa X na dhamana yake ilizuiliwa na DPP kwa madai kuwa upepelezi haujakamilika.