Wananchi wa Mkoa wa Mwanza, wameshauriwa kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi ya mara kwa mara, ili kuepukana na hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba wakati akizungumza mara baada ya kuhitimisha matembezi ya kuzuia magonjwa yasiyo ambukiza kwa watumishi na Wananchi.
Amesema kwa Mkoa wa Mwanza mwaka 2020 magonjwa yasiyo ya kuambukiza yalikuwa yanachangia kwa asilimia 6 na mwaka 2024 yalifika asilia 8 hivyo kuongezeka kwa kasi na kusisitiza kuzingatia kufanya mazoezi.

“Hata hapa ofisini asilimia zaidi ya 90 wana viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa hiyo wote tuko katika hatari na mazoezi yanasaidia vitu vingi sana,” amesema.
Aidha, ameongeza kuwa magonjwa hayo yasiyo ya kuambiza kama vile kisukari, saratani, changamoto mbalimbali za figo, magonjwa ya moyo, yote hayo yana gharama kubwa sana na yana zuilika kwa mazoezi na kubadilisha mtindo wa maisha.

“Magonjwa haya zamani tulizoea kuyaona kwa matajiri lakini sasa hata kwa maskini lakini pia tulizoea kuona kwa wenye umri mkubwa lakini kwa sasa hata chini ya miaka 30,” amesisitiza Mganga Mkuu.
“Kwa hiyo wote tuko katika hatari, tuendelee kushiriki mazoezi na niwahamasishe kujitokeza kwa wingi kufanya mazoezi,” aliongeza Mganga Mkuu.

Matembezi hayo maalumu ya kuzuia magonjwa yasiyo ambukiza kwa Watumishi na Wananchi yanalenga kuimarisha afya, yalizinduliwa rasmi Januari 18, 2025 hivyo leo ni mwendelezo na hufanyika kila jumamosi ya tatu ya mwezi.