BENKI YA DUNIA YATOA BILIONI 248 KWA SERIKALI YA TANZANIA.

Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB) wamesaini mikataba miwili (2) yenye thamani ya dola za Marekani milioni 104, sawa na takriban shilingi bilioni 248, kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia nchini Tanzania, maarufu kama “PAMOJA”. 

Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika jijini Dar es Salam kati ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete. 

Akifafanua kuhusu mikataba hiyo, Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa mkataba wa dola za Marekani milioni 4, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 9.5 ni msaada na Mkataba wa dola za Marekani milioni 100, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 238 ni mkopo wenye masharti nafuu.

Alisema mradi wa PAMOJA uliosainiwa utasaidia kuongeza upatikanaji wa fursa za kiuchumi kwa wanawake pamoja na huduma za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia Tanzania Bara na Zanzibar. 
‘’Hili litatimizwa kupitia uimarishaji vikundi vya wanawake kwa kuwajengea ujuzi wa biashara na kuwaunganisha na fursa za masoko, kuongeza fursa za mikopo nafuu kwa vikundi vya wanawake, kuwaongezea upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia mifumo rasmi ya kifedha pamoja na kuimarisha huduma za kukabiliana na ukatili wa kijinsia”, alifafanua Mhe. Dkt. Nchemba,

Alisema mradi huo utawanufaisha moja kwa moja wanawake wapatao 319,850 na walengwa wengine 399,000, wakiwemo wanafamilia za wanufaika.

Alisistiza kuwa kukuza usawa wa kijinsia si suala la wanawake pekee bali ni msingi wa Taifa la kidemokrasia, lenye haki na linalostawi na kuongeza kuwa kuondoa tofauti za kijinsia kunaboresha uzalishaji na kuimarisha uhimilivu wa kiuchumi.

“Mradi wa PAMOJA ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Taifa 2021/22 – 2025/26, Rasimu ya Dira ya Maendeleo ya 2050 na pia ni sehemu ya ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amelipa kipaumbele suala la usawa wa kijinsia”, alisema Mhe. Dkt. Nchemba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *