MKUU WA MKOA AWAONYA WANAOKWAMISHA KAMPENI YA UGAWAJI WA VYANDARUA

NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA

12 DECEMBER 2024

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewatahadharisha wananchi wa Shinyanga kuwa yeyote atakayekwamisha kampeni ya ugawaji wa vyandarua vya bure vinayolenga kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Malaria atakuchukuliwa hatua za kisheria.

RC Macha ameyasema haya leo tarehe 12 Desemba, 2024 wakati wa ufunguzi wa Kampeni ya Uhamasishaji na Ugawaji wa Vyandarua kwenye kaya bila malipo kwa Mkoa wa Shinyanga, huku akisisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -TAMISEMI pamoja na wadau (Bohari ya dawa – wasambazaji wa vyandarua na Mfuko wa Dunia unaoshughulikia Afya (Global Fund) imeandaa kampeni ya Kitaifa ya ugawaji wa vyandarua katika ngazi ya kaya ikiwa ni moja ya mikakati ya kukabiliana na ugonjwa wa malaria.

“Ninatoa tahadhari kwa wanashinyanga kuwa yeyote atakayethubutu kujaribu kukwamisha kampeni hii ya ugawaji wa vyandarua vya bure ambavyo vinalenga kudhibiti kusambaaa kwa maambukizi ya ugonjwa wa Malaria atakuchukuliwa hatua kali za kisheria kwani Serikali inafanya jitihada kubwa ili kuzuia ugonjwa huu” amesema RC Macha.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni amesema kupitia kampeni hii ya ugawaji vyandarua bure inayoambatana na utoaji wa mafunzo kwa watendaji wa afya inaenda kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa matumizi ya vyandarua majumbani kwani lengo ni kuzuia maambukizi na kutokomeza Malaria.

Naye Afisa Mradi wa Taifa wa kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya ndg. Wilfred Mwafungu ameomba ushirikiano wa pamoja kuhakikisha Kaya zote kwenye Halmashauri zote 6 za Mkoa wa Shinyanga zinafikiwa na wananchi wanapata vyandarua ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Malaria.

Serikali kupitia Wizara ya Afya inafanya jitihada kubwa kuhakikisha inapiga vita maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwani ina mpango wa kuleta vyandarua zaidi ya Milioni 1 ambapo asilimia 70 ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga watapokea vyandarua bure na hivyo kupunguza maambukizi ya ugonjwa huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *