JAMII YATAHADHARISHWA KUHUSU MADHARA YA SUMU.

Na Adam Msafiri,Mara.

JAMII nchini imetakiwa kuchukua tahadhari za kujikinga na kuepuka madhara yatokanayo na sumu ikiwemo dawa zinazotumika kwenye mimea,mifugo,kemikali zitumikazo katika uchimbaji wa madini pamoja na sumu itokanayo na kung’atwa na wadudu wenye sumu kama vile nyoka.

Rai hiyo imetolewa Desemba 12,2024 na Msimamizi wa kituo cha Taifa cha kudhibiti matukio ya Sumu Bw.Yohana Gushashi wakati akitoa mafunzo kwa maafisa afya wa wilaya,wahudumu ngazi ya jamii,wawakilishi wa wachimbaji wadogo wa madini pamoja na wenyeviti wa vijiji kutoka kata 8 za halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Aidha Gushashi amesema wamechagua kutoa elimu kwa kundi hilo wakiwemo wenyeviti wa vijiji kwani wanaamini watakua mabalozi wazuri wa kufikisha elimu kwa wananchi wao huku akisema wamechagua halmashauri ya wilaya ya Musoma kwa kuwa wananchi wa eneo hilo miongoni mwa shughuli zao mfano uchimbaji madini,unahusisha matumizi ya kemikali ya Zebaki katika uchenjuaji ambayo kwa kiasi kikubwa ni sumu na ina madhara.

“Pamoja na kwamba wanajishughulisha na shughuli za kilimo lakini pia wanafanya uchimbaji wa madini,lakini vilevile wao wapo jirani na Ziwa Victoria ambapo shughuli hizi wanazozifanya pengine zinaweza kupelekea uchafuzi wa mazingirz na hivyo kupelekea sumu za aina mbalimbali,ikiwepo sumu ya zebaki kuweza kufika katika maeneo hayo”Amesema Bw.Yohana Gushashi Msimamizi wa kituo cha Taifa cha kudhiobiti matukio ya Sumu.

Kwa upande wake Mteknolojia kutoka kituo hicho cha kudhibiti matukio ya sumu (NPCC) kilicho chini ya Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa serikali,Bi Christer Mwageni amesema hata dawa za binadamu zinaweza kugeuka kutoka kuwa tiba na kuwa sumu kama hazitatumika ipasavyo,huku akitoa angalizo dawa za kuuliwa wadudu mashambani zitumike vyema na mtumiaji ahakikishe anakua na vifaa vya kumkinga kama vile barakoa.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara,Msongela Palela amepongeza jitihada hizo za kupeleka mafunzo kwa wananchi juu ya namna ya kudhibiti na kujikinga na madhara ya sumu mbalimbali ambapo amepigilia msumari kuwa bado kuna kiwango kikubwa cha matumizi ya kemikali ya zebaki kwenye halmashauri hiyo ambayo inatumiwa zaidi na wachimbaji wadogo katika uchenjuaji wa dhahabu.

Bw.Msongela amesema“Tumepokea mafunzo haya kwa ya ajili ya udhibiti wa sumu hususan katika migodi,halmashauri yetu ya wilaya ya Musoma ina shughuli hizi za uchimbaji hivyo matumizi ya zebaki yapo kwa kiasi kikubwa,kwa hiyo tunaamini kwamba kupitia mafunzo haya wale watumiaji sasa wataelimika zaidi,lakini wenyeviti wetu na hawa wahudu wa afya watakua ni mabalozi wazuri kwa jamii.”

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo yaliyofanyika Suguti katika katika Ofisi za halmashauri ya Wilaya ya Musoma,wenyeviti wa vijiji na wahudumu wa afya wamesema sasa wanao wajibu mkubwa wa kuinusuru jamii dhidi ya matumizi holela ya dawa ambazo hugeuka kuwa sumu pamoja na kuwasaidia wachimbaji kwa kuwapatia elimu ili wachukue hatua ya kujikinga dhidi ya athari za zebaki kwa kuwahamasisha kutumia vifaa kinga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *