Watuhumiwa 23 wa dawa za kulevya Shinyanga wapandishwa kizimbani

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) wamewafikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Watu 23 wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Washitakiwa wamefikishwa mbele ya Mahakama hiyo kujibu tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi, heroin na mirungi kinyume cha Sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Sura 95 marejeo ya mwaka 2019 kifungu cha 15 A Kifungu kidogo (1) (2) na kifungu cha 17.

Akisoma Mashauri hayo 18 ya Jinai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Christina Chovenye, wakili wa Serikali John Hamenya amesema kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti katika mwezi Februari na Machi mwaka 2023 katika wilaya ya Kahama huku wakijua wazi kuwa biashara hiyo ni kosa kisheria.

Watuhumiwa wote kwa pamoja wamekana mashtaka yanayowakabili na mashauri yao yameahirishwa hadi Machi 14,15 na 26 mwaka huu kwa hatua ya kutajwa na kusikilizwa baada ya upelelezi kukamilika.

Hata hivyo, nafasi ya dhamana kwa watuhumiwa iko wazi kwa Watakaokidhi vigezo vya Mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *