Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) imesema inayoorodha ya wasanii wote wanaojihusisha na dawa za kulevya na imewataka kuacha mara moja kabla ya kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza leo Novemba 14, 2023 jijini Dar es Salaam mbele ya Wahariri wa vyombo vya habari , Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesisitiza wanayo orodha ya wasanii wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa hizo na kwamba muda sio mrefu wataanza kuchukua hatua dhidi yao.
Ametoa maelezo hayo baada ya Wahariri wanaoshiriki Semina iliyoandaliwa na Mamlaka hiyo kutaka kujua ni mkakati gani unachukuliwa katika kuwadhibiti wasanii ambao wengine ni maarufu na wanaonesha kujihusisha na dawa za kulevya waziwazi na wakati mwingine kutumia tungo zao kusifu dawa hizo.
Wakati anajibu hilo Kamishina Jenerali Lyimo amesema sheria inawaruhusu kumkamata mtu yoyote ambaye wanahisi anajihusisha na dawa za kulevya, kwenda kumpima na ikithibitika anatumia basi atafikishwa katika vyombo vya sheria.