Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Dereva bodaboda miaka 30 jela kwa kubaka mwanafunzi

Mahakama ya wilaya ya Shinyanga imemuhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani bwana Machuma Sita ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda mkazi wa Kizumbi Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kosa la kumbaka binti wa miaka 15 ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Msingi Ibinzamata.

Shauri hilo namba 146 la mwaka 2023 limeendeshwa na wakili wa Serikali Nyamnijaga Magoti na kusikilizwa mbele ya Hakimu wa Wilaya Yusuph Zahoro, huku akisema ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashitaka umethibitsha pasipo kuacha shaka kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 130 cha kanuni ya adhabu.

Akisoma ushahidi Mahakamani hapo Hakimu Zahoro amesema upande wa mashitaka umethibitisha kuwa mtuhumiwa amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi huyo tangu mwezi Aprili 2023 huku akimwingilia kwa nyakati tofauti binti huyo hadi walipokamatwa Julai 31 2023 majira ya saa tatu Asubuhi.

Amesema siku hiyo Viongozi wa Kata ya Ibinzamata akiwemo Mtendaji wa Kata, Afisa Elimu Kata na mwalimu wa Shule ya Msingi Ibinzamata walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa mwanafunzi huyo mara nyingi wakati wa masomo huwa anakwenda nyumbani kwa bwana Machuma na wanajifungia ndani ndipo walipoweka mtego na hatimaye kuwakamata.

Akijitetea kabla ya kuhukumiwa kifungo hicho bwana Machuma ameiomba Mahakama hiyo kuangalia upya suala hilo kabla ya kutoa adhabu kwani yeye alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mama wa binti huyo na baada ya kutokuelewana na mama huyo ndipo alipomtengenezea mtego huo na binti yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *