
Jeshi la Israel linaendelea na mashambulizi yake dhidi ya mji wa Rafah katika wa mpaka wa kusini wa Gaza, huku idadi ya Wapalestina waliouawa ikiongezeka na kukiwa hakuna dalili ya kupatikana kwa makubaliano ya amani.
Asubuhi ya Jumatatu Mei 13,2024, anga la Gaza lilikuwa limetanda moshi kutokana na mashambulizi ya mabomu na mizinga yaliyofanywa na jeshi la Israel, wakati likijaribu kujipenyeza ndani ya mji wa kusini wa Rafah kwa kile msemaji wake, Daniel Hagari, alichokiita kuwa ni operesheni maaluum na kuwafanya wakimbizi wa ndani wa Kipalestina kukimbia huku na kule kutoka kwenye eneo awali lilikuwa hifadhi yao ya mwisho.
Jeshi la Israel linadai kuwa mji huo ulio mpakani mwa Gaza na Misri ni ngome ya mwisho ya wapiganaji wa Kipalestina na kwamba lazima likamilishe operesheni yake ya kuwamaliza wapiganaji hao na kuwakombowa mateka waliosalia mikononi mwao.
Usiku wa Jumapili ya Mei 12,2024 jeshi hilo lilikivamia kitongoji cha Zaitun ambako lilidai kuwauwa wapiganaji kadhaa wa Kipalestina pia liliushambulia upande wa kaskazini katika kambi ya Jabalia, ambako wapiganaji wa Hamas wamejikusanya tena kwenye maeneo ambayo jeshi hilo liliwahi kudai kuwa lilishayasafisha miezi kadhaa iliyopita.
Wapalestina wapatao 300,000 kati ya raia milioni moja wanaojihifadhi huko, washameukimbia tayari mji huo kufuatia amri iliyotolewa na Israel.

Ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jeshi la Israel limewauwa Wapalestina 63 na kuwajeruhi wengine 114, na hivyo kuifanya idadi ya vifo kufikia 35,034 na majeruhi 78,755 tangu awamu ya sasa ya mapigano ilipoanza tarehe 7 Oktoba, kufuatia uvamizi wa wanamgambo wa Kipalestina dhidi ya Israel, ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200 na wengine 250 kuchukuliwa mateka.
Israel inasema imeshawauwa wanamgambo 13,000 wa kundi la Hamas hadi sasa, ingawa haijatoa ushahidi wowote unaothibitisha hilo.