WAANDAMANAJI WAAMSHA GHASIA MAREKANI, TRUMP ATUMA WANAJESHI KUDHIBITI

Vyombo vya ulinzi na usalama vya nchini Marekani, vimejikuta kwenye wakati mgumu kutuliza maadamano makubwa yanayoendelea katika jiji la Los Angeles kupinga sheria za uhamiaji zinazo lalamikiwa kukandamiza wageni, ikiwa ni sera ya Rais wa taifa hilo, Donald J. Trump.

Kwa mujibu wa shirika la habari la CNN, polisi wa Los Angeles wametumia milipuko na mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji hao, na baadhi yao kupigwa na kukamatwa.

Kwa mujibu wa mtandao wa Aljazeera, ulioripoti leo Jumatatu Juni 9 2025, ghasia hizo zilizuka jijiji Los Angeles kutokana na hatua ya waandamanaji hao ambao licha ya kufunga barabara kuu ya 101 ya jiji hilo, pia walirusha fataki na chupa za moto zilizolenga moja kwa moja vikosi vya usalama, na kusababisha uharibifu mkubwa wa magari ya polisi na ya watu binafsi yaliyokuwa eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo, kwa mujibu wa shirika na BBC, Rais Trump amepeleka wanajeshi 2,000 wa kikosi cha kitaifa (National Guard) kuimarisha ulinzi. Vile vile shirika la habari la CNN limerepoti kuwa Rais Trump anajipanga kupeleka wanajeshi wengine 500 wa kikosi cha kivita cha ‘Marines’.

Inaelezwa kuwa watu wasiopungua 27 walikamatwa Los Angeles kufuatia vurugu hizo, huku Rais Trump akiwataja waandamanaji hao kuwa ni ‘waasi waliolipwa’. Picha za machafuko, kukamatwa, kupigwa na kutiwa kizuizini kwa waandamaji hao zimeonekana kwenye mitandao ya kijamii na vyombo rasmi ya habari vya Marekani.

Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), Kash Patel, ameahidi kurejesha utulivu, akisema kuwa jiji la Los Angeles liko chini ya mashambulizi ya kihalifu na wahalifu wa mitaani.

Katika hatua nyingine, machafuko mengine yameripotiwa katika jiji la San Francisco, Kaskazini mwa California, ambapo polisi wamethibitisha kuwakamata watu wasiopungua 60 baada ya mapambano kati ya waandamanaji na maofisa wa usalama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *