Na Daniel Gahu – Katavi.
Wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi hasa wa Kitongoji Cha Rwafe kilichopo Kijiji Cha Vikonge wamelalamikia changamoto ya kufukuzwa na kukamatwa kwa Mifugo yao pindi wakipeleka mofugo yao malishoni.
Wakizungumzia kadhia hiyo, baadhi ya Wafugaji akiwemo mkazi wa Mpanda, Mishamo Joseph Kasomera ameiomba Serikali iwatengee maeneo maalum ya kulishia mifugo yao, kwani hali iliyopo sasa ni mbaya na inawafanya kuhisi wao hawathaminiki kutokana na kufukuzwa kila uchao wanapoenda kulisha mifugo.

Amesema, “Serikali itusaidie maeneo yakuchungia maana tunafukuzwa sana, Sasa sijui wanataka tuende wapi na ukizingatia wanatumia mifugo yetu kwamatumizi ya nyama mabuchani, maziwa majumbani na hata mtu akinywa masumu huko wanasema kimbilia maziwa ili sumu isimdhuru lakini hawajali hayo wao wanatufukuza tunaomba Serikali itusaidie.”
Kwa upande wake Mfugaji Magembe Emanuel Walwa, amesema kwasasa wafugaji hawasikilizwi na mifugo yao imekuwa katika hali mbaya na inakamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama, kitu ambacho huwachukua zaidi ya siku tatu kuikomboa kutoka kituoni au kushindwa kabisa kuikomboa kutokana na kuwekewa fidia ya juu kwa Kila mfugo.

“Tunanyanyasika sana utafikiri sisi sio Watanzania, unakuta Ng’ombe zikikamatwa tunafanywa dili, mtu kutoka Dar es Salaam anakuja kununua mifugo huku Rwafe kwa kupigiana simu na kutuona sisi Wafugaji hatuna akili na hata tukifika Serikalini hatusaidiwi zaidi ya kufanywa kama chambo,” alisema mfugaji Magembe
Akiongelea suala hilo, Afisa Mifugo toka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Ezediel Mhando amesema kwasasa tayari wamamaliza taratibu zote za upimaji wa maeneo ya shughuli za ufugaji chini ya usimamizi wake, kwa kutenga eneo la Ranchi ya Mifugo lenye ukubwa wa hekta 9,000 katika Kijiji Cha Vikonge kilichopo ndani ya Halmashauri hiyo.

Amesema, ugawaji wa maeneo hayo kwa shughuli ya mifugo umezingatia uwepo wa mito mingi ya Maji, kwa ajili ya kunyweshea Mifugo hiyo huku akitoa rai kwa Wafugaji hao kuepuka kulishia Mifugo katika maeneo yasiyo rasmi kwanu ni kosa kisheria.
“Niwaombe wafugaji watembelee katika Ofisi za Vijiji vyao hasa Vikonge na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, ili waweze kupatiwa maelekezo kwa kina, kwani shughuli za ufugaji hazifanyiki Kila mahali,” alisema Mhando.

Hata hivyo, ameomba Wafugaji hao kuwa waelewa na kwamba yeyote atakaye kwenda kulisha maeneo yasiyo rasmi atakuwa amkekiuka vifungu vya Sheria ya misitu ikiwemo ile ya namba 12 ya Mwaka 2012 inayotooa zuio la mtu yeyote kuingia katika Hifadhi kwenda kufanya shughuli yoyote yakiuchumi.