Na Saada Almasi – Simiyu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewataka Wananchi mkoani Simiyu kutofumbia macho vitendo vya rushwa kwa kupaza sauti pale ambapo kutaonekana viashiria, ili kutengeneza ustawi miongoni mwa jamii
Akizindua jengo la ofisi za TAKUKURU Mkoani Simiyu zilizopo katika Mtaa wa Nyaumata Wilayani Bariadi mkoani humo, Simbachawene amesema kuna namna kuongozi anaweza kutengeneza mazingira ya rushwa, hasa watumishi wa Serikali ambao hawana huduma ya bure kwa jamii na badala yake kuumiza Wananchi kila kukicha.

Amesema, “kuna hizi rushwa ndogondogo ni mbaya zaidi na zinaumiza sana watu na zaidi ni watumishi wa umma ambao wao kila huduma wanazitoa kwa malipo na bado mshahara ambao ni kodi za wananchi anakula kila mwezi tuamke kuwabaini.”
Aidha, Simbachawene amesema katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025 zaidi ya Bilioni 14 zimetumika kujenga ofisi za Taasisi hiyo nchi nzima, kutokana na umuhimu wake sambamba na kuongeza watumishi ili waweze kupenya kila sehemu ambayo kuna shughuli za kiserikali.

“Hii taasisi bado ni changa kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025 zaidi ya bilioni 14 zimetumika kujenga ofisi za taasisi hii nchi nzima lengo likiwa ni kuwafanya mpenye katika kila ofisi ya serkali mchunguze kila senti inavyotumika hata kama ofisi ya mkaguzi mkuu ipo,na pia tumeendelea kuongeza watumishi takribani 1190 hadi sasa ili kuongeza ufanisi wa kazi zenu,” ameongeza Waziri Simbachawene.
Kwa upande wake mkurugezi wa TAKUKURU Nchini, Crispin Chalamila amesema kuwa jengo hilo limejengwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria za nchi na kanuni zake licha ya kukabiliwa na changamoto kadha wa kadha kama kukosekana kwa vifaa vya ujenzi mkoani Simiyu hivyo kulazimika kufuata vifaa jijini Mwanza.

“Tunaendelea kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuweza kutuwezesha kujenga jengo hili ambalo lilijengwa kwa kufuata sheria kanuni na taratibu za nchi japokuwa tulikumbwa na changamoto hama ukosefu wa vifaa tulivyolazimika kuvifuata jijini Mwanza na kuwepo kwa mkondo wa maji na mwamba mgumu eneo hili hali iliyofanya kuchelewa kumalizika mradi kwa wakati” amesema Crispin Chalamila.
Jengo la TAKUKURU Mkoa wa Simiyu limejengwa kwa Shilingi Milioni 640 hadi kukamilika kwake, ambapo ujenzi wake ulianza Januari 5, 2023 na kukamilika Oktoba, 2023.