TUENDELEE KUILINDA, KUDUMISHA AMANI YA NCHI – DC KAGANDA

Na Afarah Suleiman, Babati – Manyara.

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, ameshiriki katika Ibada Maalum ya Kuliombea Taifa na Wilaya ya Babati, ibada iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Aldersgate ikiwa ni sehemu ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Nane wa UKWATA Mkoa wa Manyara (Easter Conference).

Ibada hiyo, imeongozwa na Mchungaji Robert Malya, Mkuu wa Jimbo la Babati kwa makanisa ya KKKT, huku ikihudhuriwa na waumini mbalimbali, viongozi wa dini, pamoja na wanafunzi kutoka shule mbalimbali zilizoshiriki katika mkutano huo wa kiroho.

Katika hotuba yake, Kaganda amewahimiza waumini na wananchi kwa ujumla kuendelea kulinda, kutunza na kudumisha amani ya nchi, kwa kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii.

Aidha, Kaganda ametoa wito kwa vijana wanaoshiriki katika mkutano huo kuzingatia maadili mema ya Kiafrika na kuishi kwa heshima, nidhamu na kuepuka matukio maovu yanayoweza kuhatarisha maisha yao na kuharibu mustakabali wa maisha yao.

Katika kuunga mkono jitihada za UKWATA, Kaganda amechangia kiasi cha shilingi milioni moja (1,000,000) kwa ajili ya uzinduzi wa gari la UKWATA Mkoa wa Manyara, mchango uliopokelewa kwa furaha na shukrani kubwa kutoka kwa viongozi wa dini na wanafunzi waliohudhuria mkutano huo.

Kaganda ameahidi kuendelea kushirikiana na taasisi za kidini na vijana katika kuhakikisha Babati na Manyara kwa ujumla vinakuwa na kizazi chenye maadili, hofu ya Mungu na kinachochangia maendeleo ya taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *