Na Saada Almasi – Simiyu.
Wakulima wa zao la Pamba Wilayani Maswa Mkoani Simiyu, wameiomba Serikali kupitia Bodi ya Pamba kuondoa changamoto iliyopo ya kuishiwa chaji mara kwa mara kwa mizani ya kupimia zao hilo pale wanapokwenda kupima pamba yao hali ambayo inawakatisha tamaa na hasara ya usafiri.
Hayo yamesemwa na Wakulima hao mbele ya wajumbe wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), iliyofanya ziara katika vijiji vya Nguliguli na Mwamenenge wilayani humo ili kujionea hali halisi ya ulimaji na uvunaji wa zao hilo sambamba na kusikiliza kero zao.
Akizungumza kwa niaba ya Wakulima hao Shija Emmanuel ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nguliguli ameipongeza Serikali kwa kuwarahisishia teknolojia hiyo na kuwataka watafute njia mbadala itakayoondoa adha ya kukatika kwa chaji ya mizani hiyo.

“Kwanza hii mizani inaturahisishia kazi ya upimaji tunashukuru sana serikali lakini ina changamoto ya kuishiwa chaji sasa unakuta mkulima naleta pamba kutoka mbali nikifika chaji imeisha ni gharama tena kurudisha pamba nyumbani tunaomba mtusaidie tupate mbadala wa chaji,” amesema Shija.
Mary John mkulima wa Mwamenenge ameishukuru bodi hiyo kwa kuondoa wizi wa kilo za zao hilo kwa teknolojia hiyo ya mzani wa kidijitali na kusisitiza suala la upatikanaji wa kitunza nishati kwa ajili ya mizani hiyo.
“Sasa hivi hata wizi wa kilo haupo kila mkulima anauza pamba yake kihalali kabisa lakini nikazie suala la kuzimika kwa sababu ya kuishiwa chaji tunaomba kitunza nishati ” power bank” iwepo ili huyu mkulima anapofika apime aondoke na hela siyo kurudi nyumbani na pamba,” amesema Mary.

Akijibu changamoto hiyo Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba, Aggrey Mwanri amesema kuwa kama bodi itahakikisha kuwa vifaa vya kuchaji mizani hiyo vinapatikana haraka ili kuondoa changamoto hizo baina ya wakulima.
“Tutashirikiana na wanunuzi kwa pamoja kuhakikisha kwamba vifaa vya kuchajia mizani yetu kama vile ‘power banks’ vinapatikana katika kila kituo chetu kwani tumegundua kuwa umeme unaotumia nguvu ya jua si mwingi sana hautoshelezi kukaa muda mrefu,” amesema Mwanri.

Naye mkurugenzi wa Bodi hiyo Marco Mtunga amewaagiza maafisa ugani BBT kutoruhusu pamba ya mkulima ambayo ni chafu kununuliwa hadi pale atakapo rudishwa na kuichambua.
“Niwape agizo maafisa ugani kama mkulima atakuja na pamba chafu msiipokee mrudisheni akaichambue ndipo afikishe hapa ipimwe,kwa sababu tunaelekeza kila siku namna bora ya uvunaji wa pamba sasa kwa nini wewe utuletee pamba chafu,” amesema Marco.


