Na Swaum Katambo – Mpanda.
Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Panta, amenusurika kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira kali baada ya kutuhumiwa kutaka kumtapeli wakala wa huduma za kifedha kiasi cha shilingi 15,000/- aliyepo katika Mtaa wa Mjimwema Kata ya Kashaulili Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Akizungumzia tukio hilo Wakala huyo, Zaburi Minyali amesema mtuhumiwa alifika ofisini kwake kutaka kutumiwa fedha kwa kutumia namba ya wakala jambo lililokataliwa na kukubaliana amtumie kupitia namba ya binafsi ya wakala.

“Nilimpa namba kisha akaondoka, baada ya muda nilimpigia simu arudi kwa kuwa hela yake imeshatumwa, alipofika chakushangaza kabla ya kutoa hela ile inakuja meseji kuwa ‘muamala uliotumwa kimakosa umerudishwa’, jambo ambalo nilihisi huyu jamaa amekuja kwa lengo la kunitapeli kwa kuwa nimeshawaji kuibiwa shilingi 167,000 kwa staili hiyohiyo” amesema Zaburi.
Hata hivyo Panta alipohojiwa alidai kuwa hafahamu kinachoendelea kwa kuwa fedha hiyo alitumwa na mwenyenyumba wake aitwaye Teddy ambaye ni mama mtu mzima na amejihisi fedheha kuambiwa kuwa yeye ni mwizi.

Mama huyo, (mwenye nyumba aliyemuagiza), Teddy akihojiwa amedai aliwasiliana na mtoto wake wa kike aliyepo Tabora na kumuomba hela ya matumizi ndipo akamuagiza mpangaji wake huyo akamtolee kupitia namba za wakala.
“Sasa baada ya muda naitwa naambiwa Panta anataka kupigwa wanasema kuwa ni mwizi ndio nikaja haraka kwa kuwa najua Panta sio mwizi mara nyingi huwa natumiwa hela na watoto wangu anakwenda yeye kunitolea kwa wakala na ananiletea,” amesema.

“tumempigia simu mwanangu aliyenitumia hela hiyo anadai kuwa yeye alimpa kijana wake anayefanya naye kazi akamsaidie kunitumia na hajui kinachoendelea, amesema kuwa anafuatilia jambo hilo” ameongeza
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamedai kuwa tukio hilo ni utapeli wa wazi kwa kuwa walimpompigia simu mtoto wa mama huyo anayesadikiwa kutuma fedha hizo aliyeko Tabora hakutoa majibu yenye kuridhisha na kukata simu.

“Mtu anakuja analia kweli anakwambia nina shida naomba unisaidie laini yangu ina changamoto, sasa ukijichanganya ukawa mwepesi na huruma yako kumsadia imekula kwako, mimi mwenyewe ilishawahi kunitokea kwenye ofisi yangu ya uwakala, nilitapeliwa shilingi laki 3 kwa staili hiihii kama aliyofanyiwa huyu bwana” amesema Mayunga ambaye ni shuhuda wa tukio hilo
Aidha wananchi hao wadai kuwa matukio ya utapeli yameshamiri hivi karibuni huku njia mbalimbali zikiendelea kuibuliwa jambo ambalo linawakosesha amani wananchi na kuchukua tahadhali kwa kushindwa kusaidiana wakidhani kuwa kila mtu ni tapeli, hivyo wameiomba Serikali kukomesha matukio hayo.