Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DK. Samia Suluhu Hassan amemhamisha kituo cha kazi aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Balozi Ali Jabir Mwadini kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa. Balozi Mwadini anachukua nafasi ya Balozi Dk. William Shelukindo ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Pia amemhamisha kituo cha kazi aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Balozi Dk. John Stephen Simbachawene kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda. Balozi Simbachawene anachukua nafasi ya Balozi Dk. Aziz P. Mlima ambaye amestaafu.
Vile vile amemrejesha nyumbani aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, Balozi John Emmanuel Nchimbi na kumteua Balozi Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri. Taarifa ya Ikulu imesema Balozi Makanzo ataapishwa Ikulu ya Chamwino Agosti 16.