Shirika la afya duniani (WHO) limesema kuwa, ugonjwa wa kisukari unaathiri idadi kubwa ya watu Barani Afrika kutokana na ukuaji wa haraka wa miji, mtindo mbovu wa maisha kama wa kukaa chini sana, utaratibu mbovu wa kula chakula pamoja na unywaji wa pombe na ulevi.

Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika Matshidiso Moeti, amesema, Bara la Afrika lina watu wazima milioni 24 wanaoishi na kisukari, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 55 ifikapo mwaka 2045.
Aidha amesema ugonjwa wa kisukari ulisababisha vifo vya watu 416,000 barani Afrika mwaka 2021, na inakadiriwa kwamba utakuwa moja ya sababu kuu za vifo barani Afrika ifikapo mwaka 2030, kama jamii za watu wa bara hilo hawatobadilisha mtindo wao wa maisha.
Asilimia 54 ya watu wanaoishi na kisukari barani Afrika hawajui kuwa wana ugonjwa huo, na wengine wengi hawajua kuwa wako katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa huo kutokana na kutopima afya zao.
Serikali za nchi za Afrika zimetakiwa kuwekeza katika jitihada za kuzuia ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kubadilisha mtindo wa maisha ya watu, utaratibu mbovu wa ulaji chakula, kupunguza unywaji pombe, kuhimiza watu kufanya mazoezi na kutoa dawa za kuokoa maisha kwa wagonjwa.