Mbunge wa Viti Maalumu Kupitia Kundi la Asasi za Kiraia Tanzania (NGOs) Neema Lugangira amesema kwamba akili mnemba (artificial intelligence – AI) ina tija na fursa nyingi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya,Kilimo na Elimu na nyenginezo hapa nchini.
Aliyasema hayo wakati akizungumza katika Semina ya Akili Mnemba kwa Wabunge Wanawake iliyoandaliwa kwa Ushirikiano na Shirika ambalo alilianzisha la Omuka Hub pamoja na Bunge la Tanzania kupitia Mradi wa Female Al Leaders chini ya Women Political Leaders (WPL) na GIZ unaolenga kuimarisha Utawala Bora wa Akili Mnemba “Artificial Intelligence #Al” kwa kuimarisha Wanawake Wanasiasa barani Afrika ili waweze kuibeba ajenda hiyo na kuwa Vinara.

Alisema katika Semina hiyo wamejadiliana mambo mengi na imeonyesha akili mnemba inafursa nyingi lakini alitoa angalizo pia isipotumika kwa usahihi ina changamoto ikiwemo ukatili wa kijinsia, kurubuni watoto na inaweza kupelekea kufifisha uwezo wa kufikiria kutokana na kutufanya sisi kuwa tegemezi sana.
“Katika semina hii, akili mnemba imetushangaza sisi kama Wabunge sababu niliamua kufanya jaribio la kuiuliza hii AI swali kuwa mimi ni Mbunge na naelekea kwenye uchaguzi, naomba inisaidie kuniandalia mkakati wa kampeni na baada ya dakika chache AI ikanipa mkakati kabambe kwa usahihi hadi mwenyewe unashangaa na inakuwa na uwezo wa muda mfupi wa kupima kila kilicho kwenye mitaandao yote yenye uwezo nayo inakupa picha pana”, Alisema Mbunge Neema Lugangira.

Alisema kwamba Akili Mnemba ni kitu ambacho kina tija lakini tija hiyo ili iweze kupatikana lazima itumike kwa ufasaha na wao kama Wabunge ni kitu ambacho wanakwenda kukiangazia; ni lazima kama Tanzania iwepo sera ya akili mnemba pamoja na sheria ili kama taifa linufaike na faida zake na pia kujikinga na kudhibiti na madhara yanayoweza kupatikana kwenye eneo hilo la akila memba.
Awali akizungumza Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu alisema niwaondolee hofu akili mnemba haijaja kupora ajira za watu bali imekuja kuboresha ajira na kukuanzisha ajira na haijaja kumbagua mtu yoyote.