Papa Francis amemfuta kazi askofu Joseph Strickland, ambaye ni mkosoaji mkubwa aliyeibua maswali juu ya uongozi wa Papa katika Kanisa Katoliki.
Askofu Strickland ni mmoja kati ya sauti kinara katika tawi la uongozi wa Kanisa Katoliki nchini Marekani ambalo linapinga vikali mabadiliko yanayopigiwa chapuo na Papa Francis.
Kuondolewa kwake kunakuja baada ya Papa kuzungumzia juu ya hali “ya kuwa nyuma” kifikra ya baadhi ya viongozi wa Kikatoliki nchini Marekani.
Askofu Strickland mara kadhaa ameshambulia hatua za Papa kutaka kubadili msimamo wa Ukatoliki katika masuala kadhaa ya kijamii ikiwemo kutoa mimba, haki za waliobadili jinsia na ndoa za jinsi moja.