Wakati wazazi na walezi wakiwaandaa Watoto kwa ajili ya mwaka mpya wa masomo, Kikosi cha Usalama Barabarani kimepiga marufuku dereva wa bodaboda kubeba mtoto chini ya miaka tisa, kwani ikibainika atachukuliwa hatua za kisheria yeye pamoja na mzazi wa mtoto huyo.
Mrakibu mwandamizi wa polisi na mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Shinyanga Wenceslaus Deus Gumha amebainisha hayo leo Januari 4 ,2024 wakati wa mahojiano maalumu na Jambo Fm, ambapo amesema wamejipanga wanahakikisha madereva wote wa vyombo vya usafiri wanafuata taratibu na sheria zote za barabarani katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wanafungua shule.
Aidha SSP Gumha amewataka wazazi na walezi pamoja na madereva wote wa vyombo vya usafiri kufuata sheria na taratibu ikiwa nia pamoja na kuacha tabia ya mazoea ya kubeba wanafunzi kwenye pikipiki na bajaji zaidi ya idadi inayotakiwa kisheria yaani mshikaki ili kulinda uhai wa watoto na madereva mwenyewe.
Katika hatua nyingine Gumha amesisitiza wananchi wote kwa ujumla kujitolea kuwavusha wanafunzi ambao hawana uwezo wa kuvuka barabara na kuwataka madereva kuheshimu haki ya watembea kwa miguu hasa katika maeneo yenye alama ya pundamilia (zebra).