Siku ya Afya ya Akili Duniani huadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 10 Oktoba kwa lengo la kuongeza uelewa wa matatizo ya afya ya akili duniani kote na kuhamasisha jitihada za kusaidia afya ya akili.
Siku hii iliadhimishwa kwa mara ya kwanza tarehe 10 Oktoba 1992, kwa ushirikiano na Shirikisho la Afya ya Akili Duniani “World Federation of Mental Health” pamoja na kuungwa mkono na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Siku hii inatoa fursa kwa wale wote wanaohusika katika ngazi mbalimbali katika nyanja ya afya ya akili kuchunguza na kubadilishana uzoefu, mang’amuzi ya masuala muhimu na mapendekezo, ili kuchangia katika kufanya huduma kwa watu wenye matatizo ya akili kuwa halisi, inayopatikana, huduma inayojumuisha pamoja na kuleta ufanisi bora duniani kote.
Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani kwa Mwaka 2023 inayonogeshwa na kauli mbiu “Afya ya akili ni haki ya binadamu kwa wote” lengo ni kuboresha ujuzi, kuongeza ufahamu na kuendesha vitendo vinavyokuza na kulinda afya ya akili ya kila mtu kama haki msingi ya binadamu ulimwengu wote.
Ikumbukwe kwamba, Afya ya akili ni haki ya msingi kwa watu wote mbapo Kila mtu, yeyote yule na popote alipo, ana haki ya kufikia kiwango cha juu zaidi cha afya ya akili.
Bado mtu mmoja kati ya wanane duniani kote anaishi na hali ya afya ya akili, ambayo inaweza kuathiri afya yao ya kimwili, ustawi wao, jinsi wanavyoungana na wengine, na maisha yao.