Daktari Dias Jumba Wabwire (31), wa Mombasa Nchini Kenya amesimamishwa kazi na Baraza la Maafisa wa Kliniki baada ya kudaiwa kumbaka mgonjwa aliyekuwa akipata huduma ya usafishaji damu katika Hospitali ya Pandya.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza hilo, Ibrahim Wako amesema tukio hilo lilitokea Januari 31, 2025 na tayari ametangaza kusimamishwa mara moja kwa leseni ya Wabwire wakati uchunguzi ukiendelea.
Daktari huyo wa figo Wabwire, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mombasa, Alex Ithuku akishtakiwa kwa ubakaji aliomfanyia mgonjwa wa dialysis katika hospitali ya kibinafsi.

Anashtakiwa kwa kumbaka mgonjwa kwa makusudi na kinyume cha sheria na pia anakabiliwa na shtaka mbadala la kitendo kichafu kwa mgonjwa, madai ambayo aliyakana na kuachiliwa kwa bondi ya Sh 500,000 na mdhamini mmoja.
Mapema hapo jana, Shirikisho la Wanasheria Wanawake-Kenya na mashirika ya kutetea haki za binadamu yalitaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu kesi hiyo ambayo imeibua hisia tofauti kwa jamii.