Daftari la kudumu la wapiga kura kufanyiwa majaribio

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kufanya zoezi la uboreshajia wa majaribio wa daftari la kudumu la wapiga kura katika kata ya Ng’ambo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoani Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara kuanzia Novemba 24 hadi 30 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 9, 2023 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Tume hiyo Ramadhani Kailima wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uboreshaji wa majaribio wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Kailima amesema zoezi hilo la uboreshaji litafanyika katika vituo 16 vya kuandikisha wapiga kura kati ya hivyo vituo 10 ni katika kata ya Ng’ambo na 6 vipo kata ya Ikoma.

Aidha, ametaja lengo la kufanya zoezi hilo kuwa ni kupima uwezo wa vifaa na mifumo ya uandikishaji itakayotumika wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura unaotarajiwa kufanyika nchi nzima kwa tarehe na ratiba itakayopangwa na tume.

Sambamba na hayo maeongeza kuwa uboreshaji huo utahusisha vyama vya siasa kwa kuweka wakala mmoja katika kila kituo cha kuandikisha wapiga kura lengo likiwa ni kushuhudia na kujiridhisha kuhusu taratibu zitakazotumika wakati wa uboreshaji wa majaribio wa daftari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *