Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), kumsimamisha kazi Meneja wa Huduma kwa wateja kwenye shirika hilo na kuweka mtu mwingine kufanya hiyo kazi.

Pia amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) kumuondoa mara moja kazini Ofisa Uhusiano na kuweka mtu mwingine kwa kushindwa kufanya kazi yake.
Biteko ametoa maagizo hayo leo Novemba 14, 2023, wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Msimbati, Halmashauri ya Mtwara, Mkoani Mtwara. Amesema Meneja wa Huduma kwa Wateja Tanesco, amekuwa akitoa majibu yasiyoridhisha kwa wateja pindi wanapopiga simu kwenye shirika kupata majibu kutokana na tatizo la umeme. Biteko ambaye alioneshwa kukerwa na mwenendo wa meneja huyo wa huduma kwa wateja amesema ni lazima watendaji serikalini wawajibike ipasavyo.