Taasisi ya chemba ya biashara Mkoa wa Shinyanga TCCIA kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imeandaa kongamano la biashara litakalowakutanisha wafanyabiashara wote na uongozi wa serikali lengo ikiwa ni kueleza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.

Kongamano hilo litafanyika kuanzia Novemba 24 hadi Novemba 26 mwaka huu katika viwanja vya hoteli ya Karena huku wafanyabiashara wakitakiwa kuchangamkia fursa hiyo kutafuta suluhu ya changamoto zao.
Makamu mwenyekiti wa TCCIA Hatibu Mgeja ameeleza hayo katika mahojiano maalumu na jambo fm ambapo amesema kupitia kongamano hilo wafanyabiashara watapaza sauti zao kwa serikali ikiwakilishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dokta Dotto Biteko ambaye anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi, akiongozwa na na viongozi wengine wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme.
Kwa upande wake katibu wa TCCIA Marcelina Saulo amesema kuwa wafanyabishara wa ngazi zote wana haki na wanaruhusiwa kushiriki katika kongamano hilo wakiwemo wajasiriamali na wafanyabishara wadogo wadogo. Kongamano hilo la TCCIA litakaloambatana na maonesho ya bidhaa za wafanyabiashara mbalimbali limeandaliwa kwa ushirikiano mkubwa wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jambo Group pamoja na Jambo Fm.