Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amemtaka mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa kusambaza umeme wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mkoa wa Shinyanga kujitahidi kutekeleza mradi huo kwa wakati uliopangwa na kwa kuzingatia ubora.
Rc Macha ameyasema hayo wakati wa utambulisho wa mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa kusambaza umeme Vijijini katika Vitongoji 90 ambao utanufaisha kaya 2970 Mkoani Shinyanga kupitia kampuni ya wazawa ya Derm Group Ltd ya Jijini Dar Es Salaam.
“Nikupongeze mkandarasi kwa kushinda zabuni hii ya kusambaza umeme kwenye Vitongoji 90 vilivyopo katika mkoa wetu wa Shinyanga lakini nikuagize kwenda kutekeleza mradi huu kwa wakati uliopangwa na kuzingatia ubora wa hali ya juu kwa sababu miundombinu ni salama na haina changamoto zozote ambazo zinaweza kukukwamisha kufanya kazi hii kwa weledi” Amesema Rc Macha.
Kwa upande wake Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi Mhandisi Robert Dulle ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa Shilingi Bilioni 11 ili zitumike kusambaza umeme kwenye Vitongoji 90 Mkoa wa Shinyanga huku akieleza kuwa tayari maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi yameanza.
Akizungumza baada ya utambulisho, Meneja wa mradi wa kampuni ya Derm Group Ltd Mhandisi Justinus Mutalemwa amesema mpaka sasa mradi huu unaendelea kutekelezwa na utakamilika baada ya muda mfupi kabla ya miezi 24 iliyopangwa kukamilika kwani hakuna changamoto zozote zilizojitokeza.
Mradi huu wa kusambaza umeme kwenye Vitongoji 90 unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 24 ambapo utekelezaji ulianza Septemba 2024 na utakamilika tarehe 19 Agosti, 2026 katika majimbo 6 kutoka Wilaya za Shinyanga, Kahama na Kishapu.