Dereva aliyesomewa makosa 64 mahakamani adai afya yake sio nzuri

Trafiki kesi namba 30855/2024 inayomkabili dereva wa basi Shedrack Swai (37) aliyesababisha ajali Oktoba 22, 2024 wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza imehairishwa baada ya mshtakiwa kuiomba Mahakama ya Hakimu Mkuu Mkazi wilaya ya Misungwi kuahirisha kesi hiyo akidai kutokuwa vizuri kiafya.

Kesi hiyo iliyokuwa imepangwa Novemba 5, 2024 kwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo Mhe. Esther Marick kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali imeahirishwa hadi Novemba 11, 2024.

Kabla ya kuanza kusomewa hoja za awali na mwendesha mashtaka wa Serikali Lilian Meli, mshtakiwa alinyoosha mkono juu ndipo Mhe. hakimu Esther Marick kuruhusu mshtakiwa azungumze.

“Mheshimiwa Hakimu, sijisikii vizuri kiafya,” alisema Mshtakiwa Shadrack Swai ambapo hakimu huyo aliridhia ombi hilo na kumpangia tarehe nyingine ili aje kusomewa hoja za awali.

“Kwa kuwa mshtakiwa ameomba kuwa hali yake kiafya siyo nzuri basi tunaahirisha shauri hili hadi tarehe 11.11.2024” amesema Hakimu.

Awali Mshtakiwa huyo alifikishwa katika mahakama hiyo Oktoba 29 mwaka huu na kusomewa mashtaka 64 kati yake tisa ni ya kuendesha gari kwa uzembe katika Barabara ya Umma Mwanza- Shinyanga na kusababisha vifo, kusababisha majeruhi, uharibifu wa mali na uhalibifu wa miundombinu kinyume na Kifungu cha 41, 63 (2) (b) na 27 (1) cha Sheria ya Usalama Barabarani namba 168 marejeo ya mwaka 2002.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Shedrack anakabiliwa na shtaka lenye makosa 64 ikiwemo kuendesha gari kwa uzembe katika barabara ya umma na kusababisha vifo vya watu tisa, majeruhi 53 na kusababisha uharibifu wa mali.

Hata hivyo, kwa sasa mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana baada ya wadhamini wake kutimiza masharti ya dhamana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *