Leah Jackson mwenye umri wa miaka 44 na ambaye ni mama watoto wanne Mkazi wa Chikole Kata ya Msalato Mkoani Dodoma amepoteza matumaini ya kuishi baada ya kidonda cha ajabu kutokea usoni mwake na kupoteza kabisa taswira ya uso, pua na mdomo.
Mwakilishi wetu katika Mkoa wa Dodoma Gideon Gregory leo Novemba 12,2024 alimtembelea mwathirika huyo nyumbani kwake ili kujionea hali halisi namna alivyo ambapo kimsingi mazingira hayaridhishi kutokana na uchumi mdogo alio nao baada ya kukimbiwa na mume wake baada ya kupatwa na tatizo hilo miaka 16 iliyopita.
Anasema alipofika katika makazi ya Leah ambaye ameishi akiwa tatizo hili kwa zaidi ya muongo mmoja na nusu ,alionekana mwenye kukata tamaa, na kupoteza tumaini, na kwa sababu ya uduni wa maisha kwani hakuwahi kupata matibabu katika vituo vya afya na badala yake amekuwa akitumia tiba za asili ambazo pia mara nyingi usanifu wake huonekana kuwa mdogo.
Leah anawakilisha kundi kubwa linalokabiliwa na changamoto za uhaba wa huduma za afya zinazosababishwa na kipato duni na baadhi yao huishia kupoteza maisha, hata hivyo sio wote wasiojua vyanzo vya maradhi yao.
Mdogo wake Leah, Dola Jackson anasema “dada yake tatizo lilianza kama kipele (chunusi) akakikwangua ndipo kikaanza kutoa damu baada ya hapo akaenda kwa masista kupata dawa alivyopatiwa hiyo dawa akapaka lakini haikumsaidia ile hali ikawa inaendelea ikabidi tutafute sehemu nyingine ndipo tukasikia kuna sehemu nyingine ya wagonjwa wa ukoma ndipo alipata dawa ambayo kidogo ilimsaidia.
Anasema baada ya hapo ile hali ilirudi tena ndipo wakaenda hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma General wakachukua ngozi ikaenda kuoteshwa Muhimbili ndipo majibu yakarudi huku yakionesha kuwa hicho ni kidonda sio Kansa.
“Kwahiyo kufikia mpaka sasa hatuna tena ratiba yoyote tunampatia tu dawa ya kumuongezea damu maana yake hatuna uwezo wa kwenda sehemu nyingine tena ya kwenda kumtibia ndugu yetu,”amesema.
Kila uchao tatizo linazidi kutamalaki, umasikini na maradhi yanazidi kuongezeka, kwani mbali na jitihada ambazo zimekuwa zikioneshwa na familia lakini bado mwangaza haujaonekana.
Mtoto wake wa kwanza wa Esau Joseph anasema kidonda hicho ni kikubwa na kimeharibika vibaya jambo linalopelekea mpaka vitu vya ndani mdomoni kuonekana.
“Hili tatizo mimi kulibeba ni kubwa sana siwezi kutokana na hali ya hapa nyumbani ilivyo, kwahiyo naomba msaada kwa watanzania wenzangu waweze kumsaidia mama kwakweli anaumwa sana naombeni msaada wenu,”amesema.
Nao baadhi ya majirani wamesema familia hiyo inapitia nyakati ngumu na kila uchwao tatizo linazidi kuwa kubwa kulingana na Leah kukosa matibabu ya kina zaidi.
Licha ya serikali kusogeza karibu huduma za afya katika jamii lakini bado baadhi ya familia hazinufaiki na huduma hizo, walimwengu wanasema kuliko kuwa na umasikini mara mbili, ni kheri ukawa na siha njema.