Benki ya CRDB imewatia nguvu waumini wa kanisa la Parokia ya Maganzo mkoani Shinyanga kwa kushiriki na katika harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Parokia hiyo.
Ndugu Madaha Chabba ambaye ni Mkuu wa Malipo na Uthibiti Benki ya CRDB akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, kwenye harambee, binafsi ametoa kiasi cha shilingi milioni 1 na laki 2 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa. Pia na Meneja Benki ya CRDB kanda ya magharibi, Jumanne Wagana ameunga mkono harambee kwa kutoa mifuko 20 ya simenti.
Akisoma hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ndugu Madaha Chabba kwenye harambee hiyo ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Parokia ya Maganzo Shinyanga tarehe 28 julai 2024 hapa chini.
“Padre Emmanuel Kahabi, Baba Paroko wa Parokia ya Maganzo
Padre John NKinga, Baba Paroko wa Parokia ya Wira
Padre Paschal Maharagu (Padre mpya kabisa wa jimbo la Shinyanga – Hongera sana)
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi Parokia ndugu yangu Gaudence Lucas
Waheshimiwa Baraza la Halmashauri Walei Parokia ya Maganzo
Viongozi wote wa Baraza la Walei toka vigango vyote ndani ya Parokia ya Maganzo.
Wageni waalikwa na Viongozi wa chama na serikali
Waumini wa Parokia ya Maganzo, shinyanga
Mabibi na mabwana,
Tumsifu Yesu Kristu…
Mungu ni Mwema………
Mhe. Baba, Paroko,na Waumini,
Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutupatia neema ya uhai na afya njema tukaweza kukutana katika Ibada hii iliyoambatana na Harambee ya ujenzi wa Kanisa la Parokia ya Maganzo
Pili, kipekee nitoe shukrani kwa Paroko na uongozi wa Parokia hii kwa heshima kubwa mliyonipa mimi binafsi kuwa mgeni rasmi katika harambee hii ya ujenzi wa kanisa. Pamoja na sababu zote ambazo katika macho ya kibinadamu zinaweza kuelezwa juu ya kwa nini mlichagua mimi kuwa Mgeni Rasmi katika jambo hili kubwa mbele za Mungu, lakini kwangu hii inabaki kuwa ni heshima kubwa ambayo sikustahili bali kwa rehema ya Mungu tu.
Aidha, niwapongeze wanaparokia wote kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuhakikisha mnakamilisha ujenzi wa kanisa hili. Hongerenisana!
Mhe. Baba Paroko naWaumini,
Siku zote nimekuwa muumini wa nukuu ya Kingereza inayosema “The man who moves the mountain begins by carrying away small stones” ambapo kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili ni kuwa“Mtu ambae huamisha mlima huanza kwa kubeba mawe madogo”.Kwa hakika, hatua hii mliofikia kama ilivyowasilishwa na paroko kwenye taarifa ya ujenzi nasadiki kusema kuwa tayari mmehamisha mlima kwa sehemu kubwa baada ya kuweza kukusanya zaidi ya kiasi cha shilingi milioni 139m ikiwa ni asilimia 45 ya lengo la kiasi shilingi milioni 308m, hongereni sana kwa jitihada hizo.
Hivyo leo hii naomba niungane nanyi katika kuwapa moyo kuwa kiasi cha shilingi milioni 169 kilichobaki hatutaweza kukifikia kwa kupitia harambee tutakayokwenda kufanya na kukamilisha safari ya kuondoa mlima wa shilingi milioni 308 mlioanza safari ya kuuhamisha kwa kuondoa mawe madogo hadi kufikia hapa mlipofikia.
Mhe. Baba ParokonaWaumini,
Katika hadithi za kwenye Biblia ambazo nimepata bahati ya kuzisikia au kuzisoma, ni ile hadithi inayopatikana Luka sura 7 aya 1 hadi 5ambayo inaeleza habari ya Akida ambae alikua akiuguza mtumwa wake aliempenda sana. Na Akida yule aliposikia habari za Yesu alituma wazee wa Wayahudi kwake kumuomba aje amponye mtumwa wake ambapo wazee wale walipofika kwa Yesu walimsihi sana wakisema “Amestahili huyu umtendee neno hili maana analipenda taifa letu naye alitujengea sinagogi”.
Kwangu mimi hili linalofanyika leo linaendana kwa sehemu kubwa na alilofanya Akida kwa kujenga sinagogi, kwani leo hii tupo hapa kwa ajili ya kukusanya fedha kupitia harambee hii ili na sisi tuweze kujenga nyumba ya Bwana kama alivyofanya mwenzetu. Hivyo nipende tu kukutia moyo ndugu yangu ambae umeshiriki harambee hii kuwa umechagua fungu jema na sote tumuombe Mungu siku moja awepo mtu wa kusimama mbele za Mungu akituombea maombi yetu na kusema “amestahili huyu umtendee neno hili mana analipenda taifa letu naye alitujengea Parokia Ya Mtakatifu Yohane XXIII
Mhe. Baba ParokonaWaumini,
Kumbukumbu ya hadithi hii ya Akida na Mtumwa wake imenipa furaha ya kupata heshima ya kuongoza harambee hii ambayo tunakwenda kutengeneza njia ya kiroho ambayo watu wanaweza kumwabudu Mungu kwa amani na utulivu.Kwangu hii ni heshima isiyoelezeka!
Nitumie fursa hii kuwaomba waumini wote kwa umoja wetu tushiriki kwa furaha katika harambee hii kama maneno matakatifu katika Wakorintho wa Pili sura ya 9 aya ya 7 na 8 yanavyosema “Kila mmoja basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha. Mungu anaweza kuwapeni nyinyi zaidi ya yale mnayohahitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema”.
Mhe. Baba Paroko,
Nnapoelekea kumaliza salamu zangu, napenda kugusia kidogo juu ya habari njema ambayo tuko nayo Benki yetu ya CRDB ambayo siku zote imekua kinara wa kuibuka na bidhaa na huduma bunifu zinazoendana na mahitaji ya makundi mbalimbali katika jamii. Kwa kutambua mahitaji ya taasisi zetu za dini, Benki yetu iliweza kuanzisha Akaunti ya Sadaka ambayo ni mahususi kwa taasisi za dini.
Akaunti hii ya Sadaka ni maalumu kwa ajili ya ukusanyaji wa michango yote ya nyumba za ibada pia haina makato ya kila mwezi, inamruhusu muumini kutoa sadaka, zaka au kulipa mchango wake akiwa popote pale nje ya kanisa. Anaweza kufanya hivyo kwa kutumia majukwaa yetu mbalimbali mfano kwenda tawini, kwa wakala, huduma zetu za kimtandao au kupitia Simbanking.
Hivyo niwakaribishe sana kutumia Akaunti hii ya Sadaka ambayo itaweza kurahisisha sana utaratibu wa utoaji wa sadaka kwa waumini na ukusanyaji wa sadaka kwa kanisa kwani hata harambee hii tunayoshiriki leo, msharika au yoyote anaetamani kushiriki awe ndani au nje ya nchi anaweza kufanya hivo kwa urahisi kupitia akaunti hii.
Baada ya kusema hayo,naomba sasa kwa heshima na taadhima nitamke kuwa nimefungua rasmi harambee hii ya kuchangia ujenzi wa kanisa letu na kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela naomba kuwasilisha ahadi yake ya Shilingi Milioni 8 kwa ajili ya harambee hii ambayo itawekwa moja kwa moja kwenye akaunti ya ujenzi ambayo imeshafunguliwa benki ya CRDB.
Asanteni kwa kunisikiliza!“
Baada ya kusoma hotuba hiyo, Chabba amesema maagizo ya Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela kuwa ametoa ahadi ya kiasi cha Shilingi Milioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa la Parokia ya Maganzo – Shinyanga.
Kwa upande wao Mapadre, viongozi na waumini wote wa kanisa la Parokia Maganzo wamejitoa kwa kuchangia katika ufanikishaji wa ujenzi wa kanisa lao
Kwa dhati, viongozi wote wa kanisa la Parokia la Maganzo wametoa shukrani zao kwa Benki ya CRDB kwa kuendelea kuonyesha upendo na kujali watu na ndio maana ni Benki inayosikiliza.