Naibu Mkuu wa Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa TAKUKURU Mkoa wa Geita Alex Mpemba amewataka wananchi Mkoani humo kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya rushwa kwa kufichua wanasiasa wanaotafuta uongozi kwa kutoa rushwa kwa wananchi.
Amebainisha hayo wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Geita ambapo amesema kuwa ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha kuwa uongozi unapatikana kwa njia halali na si kwa kutoa hongo hivyo wananchi wakibaini viongozi wa namna hiyo watoe taarifa mapema kwa Mamlaka hiyo ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Aidha Pemba amesema katika jitihada za kudhibiti matumizi mab aya ya fedha za umma, TAKUKURU Mkoa wa Geita imefuatilia miradi 25 ya maendeleo ambapo kati ya hiyo imehusisha sekta ya elimu,maji, na afya yenye miradi 5 kwa kila sekta husika huku miradi 4 ikihusisha sekta ya miundombinu ya barabara, pamoja na mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi yote yenye thamani ya shilingi bilioni 10.2.
Mpemba ameongeza kuwa kati ya miradi hiyo 25 miradi 5 imekutwa na mapungufu makubwa ambayo yanahitaji kurekebishwa ili kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika ipasavyo kwa kuwanufaisha wananchi.
Hata hivyo Mpemba ametumia nafasi hiyo kuwataka Wakazi wa Mkoa wa Geita kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa TAKUKURU pale wanapoona viashiria vya rushwa ili kuimarisha uwajibikaji na uadilifu katika uongozi na matumizi ya rasilimali za umma.