Serikali mkoani Shinyanga imemuagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Ibadakuli kuzingatia viwango na ubora kulingana na thamani ya fedha na kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa wakati kwa mujibu wa mkataba ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya usafiri wa anga .
Akikagua ujenzi wa uwanja huo mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amemtaka mkandarasi anaetekeleza mradi huo kuwapa kipaumbele wananchi wazawa wa maeneo hayo katika suala la ajira ili waweze kunufaika na uwepo wa utekelezaji wa mradi huo katika maeneo yao.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo unaotekelezwa na mkandarasi Chinahannan International Corporation Group (chico) kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 52 meneja wa wakala wa barabara (tanroads) mkoa wa Shinyanga Mibara Ndilimbi amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi november mwaka 2024.
Wakizungumzia hatua za upanuzi wa uwanja wa ndege wa Ibadakuli meneja miradi kutoka kampuni ya Chico Shi Yinlei amesema wamejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.