Rais Samia Suhuhu Hassan amesema ni muhimu Afrika kuamua sasa kwa pamoja kuwekeza mkakati wa kutangaza utalii wa Afrika, tafiti na uchambuzi wa takwimu za sekta hiyo kiuchumi pamoja na kutunza na kuhifadhi utajiri wa sekta hiyo.
Rais Samia ameyasema hayo wakati wa hotuba yake ya dakika 10 katika mkutano wa 23 wa Kimataifa wa Baraza la Utalii Duniani (WTTC) mwaka 2023, unaofanyika Kigali Rwanda.
Kuhusu mkakati wa kujitangaza, Rais Samia ameshauri sekta binafsi kushiriki katika uwekezaji ikiwamo wa filamu kwa kushirikisha watu maarufu pia kutumia simulizi za uzuri wa afrika na kupiga vita maudhui yanayochafua bara la Afrika kwa lengo la kudhoofisha mchango wa sekta hiyo.
Kongamano hilo linafanyika ikiwa ni zaidi ya miaka 30 imepita tangu baraza hilo lilipoanza shughuli za tafiti juu ya athari za kiuchumi za usafiri na utalii katika nchi 185 kwa kutazama msongamano wa watu, kodi pamoja na utungaji sera ili kukuza mchango wa sekta hiyo kiuchumi duniani.
Kwa upande wake Rais wa WTTC, Julia Simpson ameshauri viongozi wa afrika kufanya mapitio ya sera zitakazosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika shughuli za utalii duniani.
Amesema ripoti zinaonyesha mwaka 2019 sekta ya usafirishaji ilichangia asilimia 40 ya uzalishaji wa kaboni kwa uchomaji wa mafuta.