Mahakama ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imemuhukumu Theresia Kapalata (40) mkazi wa Mhungula kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kumfanyia ukatili wa kutelekeza na kumsababishia maradhi mtoto aliyekuwa akiishi naye mwenye umri wa miaka saba.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Christina Chovenye, akisoma hukumu hiyo amesema mtuhumiwa alikuwa mhudumu wa Grosery iliyopo Mwendakulima na aliomba kuishi na mtoto huyo kutoka kwa kaka yake, ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo kwa lengo la kuishi naye baada ya mama wa mtoto kufariki dunia.
Hakimu Chovenye amesema mahakama imejiridhisha na ushahidi wa upande wa mashitaka, ambao ni majirani, mwenyekiti wa mtaa na daktari kueleza alivyokuwa akitelekezwa na hakuna huduma yoyote na kusababisha apate ugonjwa wa ngozi kwa kukosa matunzo.
Amesema mahakama imeona kulingana na kosa hilo alipe faini ya Sh 500,000 au kwenda jela miaka mitatu, ambapo hakuwa na fedha hizo hivyo kupelekwa kutumikia adhabu hiyo.