Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew amesekitishwa na mwenendo wa ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 unaojengwa Kijiji cha Senga Kata ya Senga wilayani Geita Mkoani Geita kutokana na kusuwasuwa kwa ujenzi wa mradi huo hali ambayo inapelekea mradi huo kuchelewa kukamilika na kusababisha wananchi kukosa huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao.
Mhandisi Kundo amesema hayo baada ya kufanya ukaguzi wa mradi huo unaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 124 na kujionea maendeleo mabovu ya utekelezaji wa mradi ulioaanza kujengwa tangu mwezi Aprili 2023 ukitarajiwa kukamilia 2025 lakini mpaka sasa upo asilimia 18 pekee na kumtaka Mkandarasi anayejenga mradi huo M/S AFCONS kufanya kazi usiku na mchana pamoja na kuongeza wafanyakazi wa kutosha ili kuweza kukamilisha ujenzi wa mradi huo mapema.
Aidha Mhandisi Kundo amemuagiza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Geita na Mkurugenzi na GEUWASA kufanya ufatiliaji wa ujenzi wa mradi huo mara kwa mara ili kumsimamia Mkandarasi huo kumaliza mradi huo kwa wakati.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA) Frank Changawa amesema mradi huo ukikamilika utahudumia vijiji 19 katika wilaya ya Geita pamoja na Kata zote 13 za Halmashauri ya Mji wa Geita na pindi utakapo kamilika changamoto ya ukosefu na utoshelevu wa maji katika mkoa wa Geita utakuwa umeisha.
Nao baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Senga wameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa mradi huo kwani kwa sasa wanapata changamoto ya kutumia maji yasiyo salama ambayo yamekuwa yakiwasababishia magojwa mbalimbali yanayohatarisha usalama wa afya zao.