Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga limemkamata aliyeiba mtoto wa miezi 9 Kahama

Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga linamshikilia Maduki Nyembe Sabuni Mkazi wa Kijiji cha Imalanguzo Kata ya Ushirombo Halimashauri ya Wilaya ya Geita kwa tuhuma za kuiba mtoto wa miezi tisa Meresiana Paschal maeneo ya Manzese katika Manispaa ya Kahama.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi amesema tukio hilo lilitokea Julai 18 mwaka huu ambapo mama wa mtoto huyo Magdalena Sulas alikuwa akifanya shughuli za kiuchumi katika eneo la stand ya mabasi yaendayo kakola akiwa na mtoto huyo ambaye alikuwa akicheza eneo jirani kabla ya mtuhumiwa kutekeleza tukio hilo.

Aidha Jeshi hilo limesema kuwa halitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atayehusika na vitendo vya namna hiyo huku likiwataka wazazi na walezi kuwa makini na uangalizi wa karibu wa watoto wao.

Katika siku za hivi karibuni kumeibuka wimbi la upotevu wa watoto katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambapo kwa Mkoa wa Shinyanga hili ni tukio la pili na la kwanza lilitokea katika Kata ya Ndembezi Halimashauri ya Manispaa ya Shinyanga baada ya mtoto kuibiwa na mpangaji aliyekwenda kupanga katika nyumba aliyokuwa akiishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *