Kamanda wa Polisi wa Mkoa Wa Mjini Magharibi Unguja Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Richard Thadei Mchomvu amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta wahalifu waliohusika na tukio la kuvunja makazi ya watu na kuwashambulia kwa mapanga huko Dole na Mwanyanya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Kamanda Mchomvu amesema tukio hilo ambalo si la kawaida kutokea hivyo wanaendelea kufatilia kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama ili kuwakamata wahusika wote wa tukio hilo ambalo limetokea majira ya saa 8 usiku Disemba 31, mwaka 2023.
Amesema Vijana hao wanakadiriwa kufikia 15 walivamia nyumba sita katika eneo la Dole na Mwanyanya kwa nyakati tofauti na kuanza kuwapiga mapanga wakazi wa nyumba hizo na kuiba vitu mbalimbali ikiwemo laptop, simu 18 na fedha taslimu 85,0000 pamoja na kusababisha majeruhi ya watu wane.