Na Gideon Gregory, Dodoma.
Wizara ya Fedha imekutana na washirika wa maendeleo kwa ajili ya kutathmini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na kuweka mikakati ya Dira mpya ya 2050.
Kikao hicho, kimefanyika Februari 21, 2025 Jijini Dodoma ambapo kimelenga kujadili namna bora ya kuendeleza miradi ya maendeleo na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo.
Akiwasilisha hoja katika mkutano huo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil amesema, Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Mfano mzuri ni maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, ambayo sasa inatoa huduma kwa ufanisi zaidi, hivyo kuchochea biashara na uchumi wa nchi,” amesema Dkt. Akil.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR ni hatua muhimu katika kuboresha sekta ya usafirishaji, huku miradi mingine kama Bwawa la Mwalimu Nyerere ikitarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme na kuimarisha uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia Mipango ya Kitaifa, Dkt. Mursal Milanzi, amesema majadiliano na washirika wa maendeleo yanalenga kuhakikisha kuwa vipaumbele vya taifa vinaungwa mkono kwa rasilimali na utaalamu unaohitajika.
“Katika mikutano kama hii, tunakubaliana kuhusu vipaumbele vya maendeleo vya nchi na namna ya kuvitekeleza kwa kushirikiana na wadau wetu wa maendeleo,” ameeleza Dkt. Milanzi.

Kuhusu mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kukuza uchumi wake kwa kutumia rasilimali zilizopo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya madini, kilimo, viwanda, na usafirishaji.
“Tunahitaji kutumia kikamilifu nafasi ya kijiografia ya nchi yetu kwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji ili kuongeza faida kutoka kwa biashara za kimataifa na usafirishaji wa bidhaa kwa nchi jirani,” amesema.

Aidha, amesisitiza kwamba Dira ya Maendeleo ya 2050 inalenga kuongeza ajira, kukuza uchumi, na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa Wananchi wote.
Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, inaendelea kuweka mikakati madhubuti, ili kuhakikisha kuwa dira hiyo inatekelezwa kwa mafanikio.