WAZEE WANAPASWA KULINDWA DHIDI YA VITENDO VYA KIKATILI – RC MACHA

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha ameiasa jamii kuwalinda wazee kwani ni tunu ya Taifa na kwamba Serikali imeendelea kuwajali pamoja na kuimarisha ulinzi wa kutosha dhidi yao.

RC Macha amebainisha hayo Juni 14, 2025, wakati akitoa hotuba kwenye ufunguzi wa Kongamano la siku moja lililiofanyika katika ukumbi wa chama cha mapinduzi mkoa wa Shinyanga ili kujadiliana juu ya changamoto zinazowakabili wazee , katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya kupinga ukatili kwa wazee Juni 15, 2025 ambapo kitaifa yanafanyika mkoani Shinyanga.

Amesema, “Serikali itaendelea kuwa thamini wazee, kuwatimizia mahitaji yao pamoja na kuwalinda,zamani hapa Shinyanga kulikuwa na tatizo la mauaji ya wazee kwa kukatwa mapanga sababu ya Imani potofu za kishirikina,lakini sasa hivi hakuna tena na imabaki kuwa historia.”  

Aidha RC macha mesema, Serikali pia itaendelea kuboresha huduma za matibabu kwa wazee, pamoja na upatikanaji wa madawa ya magonjwa ya wazee,na kuendelea kutengwa madirisha ya wazee kwenye huduma Zote za afya, na uwekwaji wa mabango ya mpishe mzee apate huduma kwanza.

Katika hatua nyingine, amewataka vijana kuwatunza wazee wao,na kuacha tabia ya kuwatelekeza pamoja na kuwaachia wajukuu,huku wakijua kabisa hawana nguvu tena za kufanya kazi.

Awali, Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu amewasisitiza vijana wasiwaone wazee wao kama mzigo,bali ni baraka na hazina kwao,ambapo wanapaswa kuwatumia na kuchota busara zao,na kwamba wazee ni Tunu ya Taifa hivyo wasifanyiwe ukatili.

Kongamano hilo limehudhuriwa pia na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda ambaye amesema wazee kwa nchi nzima wapo Milioni 3.5, na kwamba hiyo ni hazina kubwa kwa Taifa ambayo inapaswa kulindwa.

Lakini pia meneja program wa uhusiani wa wadau na mawasiliano  wa shirika la kuhudumia wazee la Help Age Tanzania Joseph Mbasha,amesema Jamii inayothamini wazee ni yenye uhai na maadili,na kusisitiza kwamba wazee walindwe na kutimiziwa mahitaji yao,ikiwamo kuboreshwa kwa sera ya wazee ya 2003,kuongezwa kwa bajeti za wazee pamoja na kulipwa Pesheni Jamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa David Sendo amesema Kongamano hilo liwe ni sehemu ya kuleta mapinduzi na kubadilisha maisha ya wazee, sababu wao licha ya kulipigania taifa hili,lakini wamekuwa wahanga wakubwa wa matukio ya ukatili,kukosa matibabu ya uhakika,vipato,pesheni jamii na sheria ya wazee.

Amesema wanahitaji kutekelezewa mahitaji yao yote, pamoja na kuacha kubaguliwa kwa kunyang’anywa mali kama vile ardhi na kudhurumiwa nyumba,huku wakikipongeza Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa kuingiza masuala ya wazee kwenye Ilani yao ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030.

Kauli Mbiu ya Kongamano hilo ni “Wazee ni hazina kwa Taifa, tuwalinde na tuwatunze.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *