Na Ibrahim Rojala,Shinyanga
Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 209,951 likiwa ni ongezeko la asilimia 21 ya wapiga kura 995,918 waliopo katika daftari la kudumu la wapigakura hatua itakayouwezesha mkoa wa Shinyanga kufikisha idadi ya wapiga kura 1,205,869.
Mkurugenzi wa huduma na Sheria kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)Bw. Mtibohora Selemani amebainisha hayo wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa Tume na wadau wa Uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura mkoani Shinyanga uliofanyika Agosti 10,2024 ambapo pia amefafanua kwamba kwa mkoa wa Shinyanga jumla ya vituo 1,339 vitatumika katika uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 122 kati ya vituo 1217 vilivyotumika kwenye uboreshaji wa mwaka 2019/2020.
Katika hatua nyingine Bw. Selemani amewataka vijana nchini kuwa makini katika matumizi ya mitandao ya kijamii na kujiepusha na upotoshaji wa mwenendo wa zoezi la maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura hali inayoweza kuathiri ufikiwaji wa malengo ya zoezi hilo.
Awali akifungua mkutano wa tume ya wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura uliofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Mbarouk Mbarouk amesema lengo la mikutano hiyo ni kupeana taarifa za maandalizi ya kuanza kwa zoezi uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linalojumuisha uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura,uboreshaji wa majaribio,ununuzi wa vifaa na ushirikishwaji wa wadau.
Aidha amebainisha kwamba Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ilizindua zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Kigoma Julai 20 mwaka huu na kwasasa zoezi hilo linaendelea katika Mikoa ya Kagera na Geita hadi Agosti 12,2024 na mzunguko wa tatu wa maboresho hayo utafanyika katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga kuanzia Agosti 21 hadi 27 na kueleza kwamba uboreshaji huo unamhusu kila mwananchi aliye na sifa za kupiga kura na kuwataka wadau waliohudhuria mkutano huo kuwahimiza wananchi kupitia majukwaa ya kisiasa,kijamii,kiutamaduni na kiimani na kiuchumi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftrari la kudumu la wapiga kura.
Wakichangia maoni yao kupitia mkutano huo, baadhi ya washiriki wa mkutano huo wametoa wito wa kusikilizwa na kufanyiwa kazi kwa maoni yaliyotolewa kuhusiana na mchakato huo,wakiipongeza tume huru ya Taifa ya Uchaguzi na kuhimiza urekebishwaji wa baadhi ya kasoro ili kuwezesha uwepo wa uchaguzi huru na wa haki pamoja na kuitaka tume kuwasisitiza maafisa uandikishaji umuhimu wa kuzingatia kuandika kwa usahihi majina ya wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura ili kuepusha mkanganyiko unaoweza kujitokeza.
Miongoni mwa mambo mapya yaliyoongezeka katika utaratibu wa uandikishaji wapigakura kwa mwaka huu ni pamoja na uwepo wa utaratibu wa kuandikishwa wafungwa wa magereza na mahabusu(wanafunzi wa vyuo vya mafunzo kama inavyofahamika Zanzibar) utaratibu ambao umewekwa kwa mujibu wa kanuni ya 15 (2)(c) ya kanuni za uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura za mwaka 2024 ambazo zimeweka utaratibu wa kuwezesha wafungwa/wanafunzi waliohukumiwa kifungo cha chini ya mwezi sita na mahabusu kuandikishwa kupiga kura.
Ili kuhakikisha lengo hili linafanikiwa,Tume Huru ya Uchaguzi imetenga vituo vya kuandikisha wapiga kura 130 vilivyopo kwenye magereza na kwa Zanzibar kuna vituo 10 vilivyopo kwenye vyuo vya mafunzo.
Na ili kufikiwa kwa malengo,Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi imefanya maandalizi mbalimbali kitaifa ikiwa ni pamoja na vituo 40,126 vya kuandikisha wapiga kura vitakavyotumika katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kati ya hivyo vituo 39,709 vipo Tanzania Bara na vituo 417 vipo Zanzibar kukiwa na ongezeko la vituo 2,312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika mwaka 2019/2020.
Kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya watu na Makazi ya Mwaka 2022,wapigakura wapya 5,586,433 wanatarajiwa kuandikishwa ikiwa ni sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/2020,wapigakura 4,369,531 wakitarajiwa kuboresha taarifa zao na wapigakura 594,494 wakitarajiwa kuondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye daftari hivyo baada ya maboresho inatarajiwa kuwa daftari litakuwa na Jumla ya Wapigakura 34,746,638.