WANAWAKE, WASICHANA NA WATOTO 192 WAMERIPOTIWA KUPITIA UKATILI WA KIJINSIA KISHAPU.

NA EUNICE KANUMBA – KISHAPU, SHINYANGA.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amewataka watumishi wa Kituo cha Huduma Jumuishi (One Stop Centre) kilichopo wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, kutunza siri za manusura na wahanga wa ukatili wa kijinsia wanaokuja kutoa taatifa na kupatiwa huduma katika kituo hicho huku akitoa wito kwa wananchi wilayani humo kukitumia kikamilifu ili lengo la kutokomeza vitendo vya kikatili viweze kuisha kabisa. 

RC Macha ameyasema haya leo tarehe 16 Desemba, 2024 wakati akizindua kituo hicho ambacho kimejengwa kwa ufadhili wa serikali  ya Finland kupitia Shirika la Kimataifa linaloshughulikia idadi ya watu pamoja na masuala ya uzazi  (UNFPA) katika mradi wa chaguo langu haki yangu  ambapo kituo hicho  kitatoa huduma za matibabu, sheria  na ushauri wa kisaikolojia kwa manusura na wahanga wa ukatili wa kijinsia  

“Niwatake ninyi watumishi wa kituo hiki kuhakikisha kuwa mnatunza siri zote za manusura na wahanga wa vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia wanaokuja hapa nakupatiwa huduma zenu, na hili agizo ni sehemu ya viapo na maadili yenu ya kitaaluma,” – RC Macha.

Kwa upande wake mwakilishi mkazi wa UNFPA Tanzania  Mark Bryan Schreiner amesema kuwa Shirika lao litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa  masuala ya ukatili yanatokomezwa pamoja na kuyalinda makundi maalum yakiwemo ya wanawake na watoto katika Mkoa wa Shinyanga na Tanzania kwa ujumla. 

Lakini pia mkuu wa ushirikiano wa ubalozi wa Finland nchini Tanzania, Juhana Lehtinen  amempongeza RC Macha kwa utendaji kazi wake huku akiishukuru zaidi Serikali ya Tanzania kwa kuendelea na mikakati ya utokomezaji wa ukatili wa kijinsia kwa wananchi wake na kupongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Shinyanga (SHIVYWATA) kwa kuendelea kuwaunganisha walengwa wote.

Kwa ujumla, Ukatili wa Kijinsia ni pamoja na kitendo kinachofanywa dhidi ya mtu kwa sababu ya kijinsia yake. Wanaume na wanawake wanaweza kupitia ukatili wa kijinsia, lakini manusura na wahanga wengi zaidi ni wanawake, wasichana na watoto ambapo kuanzia Machi 2024 hadi Desemba 2024 kumeripotiwa takribani vitendo 192 katika Kituo hiki cha Kishapu pekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *